Dec 13, 2020 07:36 UTC
  • UN yailaumu Marekani kwa msimamo wake kuhusu Sahara Magharibi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameilaumu Marekani kwa kutangaza kulitambua rasmi eneo la Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco.

António Guterres amesema kuwa, umiliki wa eneo la Sahara Magharibi si kitu cha kutambuliwa rasmi na nchi fulani, kwani maazimio ya Umoja wa Mataifa ndiyo yenye kauli ya mwisho kuhusu eneo hilo.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kama tulivyosema kwa uwazi huko nyuma, msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sahara Magharibi haujabadilika na umebakia kama ulivyo. Uamuzi wa Trump wa kutambua kwamba eneo hilo ni mali ya Morocco hauna mashiko yoyote ya kisheria, bali maazimio ya Umoja wa Mataifa ndiyo yanayoamua haki ni ya nani katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, msimamo wa Guterres kuhusu Sahara Magharibi haujabadilika na kwamba azimio la mwisho la Umoja wa Mataifa nambari 2548 kuhusu Sahara Magharibi, ndilo la kuzingatiwa.

Sahara Magharibi

 

Juzi Ijumaa, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa Washington inatambua rasmi kwamba eneo la Sahara Magharibi ni milki ya Morocco, ikiwa ni kujaribu kuhalalisha uamuzi wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Uamuzi huo umelaaniwa vikali kimataifa. Morocco ni nchi ya nne ya Kiarabu ambayo mwaka huu imetangaza kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za Waarabu na Waislamu na hasa Wapalestina wasio na hatia.

Tags