Dec 17, 2020 04:37 UTC
  • Baraza la Usalama lataka mamluki wote waondoke nchini Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuondoka mara moja mamluki na wapiganaji wote wa nchi ajinabi nchini Libya.

Taarifa ya pamoja ya nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama imesema kuwa, kuondoka nchini Libya wapiganaji wa nchi ajinabi kunaoana na makubaliano ya usitishaji vita uliofikiwa na pande zote hasimu za Libya mnamo Oktoba 23, na pia maafikiano ya washiriki wa Kongamano la Berlin na maazimio kadhaa ya taasisi hiyo ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres anatazamiwa kuwasilisha mapendekezo ya kuundwa mikakati ya kutathmini makubaliano hayo ya usitishaji vita kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Disemba.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya, hivi karibuni ilitoa taarifa kulaani hatua ya Imarati ya kusajili mamluki nchini Sudan kwa ajili ya kuwapeleka vitani nchini Libya.

Baadhi ya mamluki waliokamatwa Sudan wakijaribu kuelekea vitani Libya

Imarati ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa kundi la jenerali muasi, Khalifa Haftar linalojiita Jeshi la Taifa la Libya.

Kwa sasa Libya ina serikali mbili; moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali nyingine ina makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi, inayoungwa mkono na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.  

 

Tags