Feb 20, 2021 12:45 UTC
  • Morocco yashadidisha ukandamizaji baada ya kuanzisha uhusiano na Israel

Serikali ya Morocco imeshadidisha mbinyo, ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wanaharakati na wananchi wa kawaida nchini humo, baada ya Rabat kukubaliana na utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzisha uhusiano wa pande mbili.

Hayo yameripotiwa na tovuti ya habari ya Middle East Eye ambayo imeeleza bayana kuwa, dhulma na kamatakamata dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na wakosoaji wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo viliongezeka kwa kiwango kikubwa kufuatia hatua ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump ya Disemba 10 mwaka jana, kutangaza kuwa Washington inatambua rasmi kwamba eneo la Sahara Magharibi ni milki ya Morocco, ikiwa ni kujaribu kuhalalisha uamuzi wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mahmoud Lemaadel, mmoja wa wanaharakati wa kisiasa huko Sahara Magharibi amesema eneo hilo limerekodi idadi kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa ya kukandamizwa wapinzani na wanaharakati katika eneo hilo katika kipindi cha wiki chache zilizopita. 

Kijana akichoma moto bendera ya Israel katika maandamano ya kupinga uhusiano na Tel Aviv

Mwezi uliopita pia, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilikosoa hali ya haki za binadamu nchini Morocco na kutangaza kuwa, maafisa wa nchi hiyo wamezidisha mbinyo na ukandamizaji wa uhuru wa raia.

Tarehe 22 mwezi Disemba mwaka jana Morocco na utawala haramu za Kizayuni wa Israel zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano baina yao na kisha Marekani ikatambua rasmi mamlaka ya udhibiti wa Morocco kwa eneo la Sahara Magharibi. 

Morocco ni nchi ya sita ya Kiarabu baada ya Jordan, Misri, Imarati, Bahrain na Sudan  kuanzisha uhusiano kati yake na utawala ghasibu wa Kizayuni. 

Tags