Apr 01, 2021 02:15 UTC
  • Morocco yakandamiza maandamano ya kuliunga mkono taifa la Palestina

Serikali ya Morocco imekandamiza maandamano ya wananchi wa nchi hiyo kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina, ikiwa ni hatua ya kwanza kabisa ya kuzuia kulaaniwa utawala wa Kizayuni nchini humo tangu Rabbat ilipotangaza uhusiano wa kawaida na Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, polisi wa Morocco wamekandamiza maandamano ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kuungana na Wapalestina katika maadhimisho ya Siku ya Ardhi. Mbali na kuliunga mkono taifa la Palestina, maandamano hayo yalikusudia kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini polisi wameingilia kati na kuyakandamiza.

Hatua hiyo ya polisi wa Morocco imewakasirisha Waislamu wa nchi hiyo na waandamanaji walibadilisha nara zao na kuanza kulaani kitendo cha utawala wa kifalme wa nchi hiyo cha kujidhalilisha kwa Wazayuni na kutangaza kwake uhusiano wa kawaida na watenda jinai Wazayuni ambao mikono yao imejaa damu za Waarabu na Waislamu hasa Wapalestina.

Mbali na Morocco, watawala hawa watatu wa nchi za Kiarabu nao wametangaza uhusiano wa kawaida na Israel

 

Tarehe 10 Disemba 2020, Morocco ilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kuungana na nchi nyingine za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan ambazo nazo zimejidhalilisha kwa Wazayuni kwa kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel na kudharau waziwazi malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

Ikumbukwe pia kuwa, tarehe 30 Machi ni Siku ya Ardhi huko Palestina. Siku hiyo imepewa jina hilo kukumbuka jinai za utawala wa Kizayuni za tarehe 30 Machi 1976 wakati utawala huo gharibu ulipowapora Wapalestina maelfu ya hekta za ardhi zao katika eneo la al Khalil la kaskazini mwa Palestina.

Tags