Apr 09, 2021 15:52 UTC
  • Msumbiji yatuma timu ya madaktari kutambua wahanga wa shambulio la kigaidi huko Palma

Msemaji wa jeshi la Msumbiji amesema kuwa nchi hiyo inatuma timu ya madaktari ili kutambua miili ya watu 12 waliouawa katika shambulio la magaidi wenye uhusiano na kundi la Daesh katika machimbo ya gesi asilia kwenye mji wa Palma kaskazini mwa Msumbiji.

Wahanga hao wasiopungua 12 wanaaminika kuwa raia wa kigeni ambao waliuawa mwezi uliopita katika shambulio la magaidi wakufurishaji wenye mfungano na kundi la Daesh katika mji wa Palma mkoani Cabo Delgado nchini Msumbiji. 

Msemaji wa jeshi la Msumbiji Chongo Vidigal ameongeza kuwa, wahanga wa mauaji hayo wanaaminika kuwa ni raia wa kigeni ingawa taarifa hiyo bado haijathibitishwa. 

Magaidi katika mji wa Palma nchini Msumbiji 

Mji wa Palma ulio karibu na mradi mkubwa ya gesi wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 60 na ambao ni makao makuu ya kampuni kadhaa za kigeni ulilengwa na mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha tarehe 24 mwezi Machi mwaka huu.  

Msemaji wa jeshi la Msumbiji jana Alhamisi alithibitisha kuwa wahanga wa mauaji hayo ni wazungu, na kwamba hata hivyo wameshindwa kuthibitisha uraia wa nchi zao kutokana na miili yao kuharibika.

Tarehe 5 mwezi huu Jeshi la Msumbiji limetangaza kuwa limeukomboa kikamilifu mji wa Palma wa fukwe za kaskazini mwa nchi hiyo katika mpaka wa Msumbiji na Tanzania.

Palma, Msumbiji

Makumi ya raia waliuawa na wengine wasiopungua 11,000 walikimbia makazi yao baada ya wanamgambo hao kuuvamia mji huo wa Palma mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi.

Tags