Apr 10, 2021 12:32 UTC
  • Jeshi la Msumbiji laua magaidi 36 katika mji wa Palma

Msemaji wa jeshi la Msumbiji amesema askari wa nchi hiyo wamewaangamizi makumi ya wanamgambo katika operesheni ya usalama katika mji wa pwani wa Palma, kaskazini mwa nchi.

Brigedia Chongo Vidigal amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari na kuogeza kuwa, magaidi wasiopungua 36 wameuawa katika operesheni hiyo ya usalama, na kwamba huenda idadi ya vifo hivyo ikaongezeka.

Ameeleza bayana kuwa, serikali ya nchi hiyo inaamini kuwa, kutumwa jeshi katika mji huo wa pwani uliokuwa umetekwa na kudhibitiwa na magaidi kumefikia malengo yake na kuzaa matunda.

Tarehe 5 mwezi huu jeshi la Msumbiji lilitangaza kuwa limeukomboa kikamilifu mji huo wa Palma wa fukwe za kaskazini mwa nchi hiyo katika mpaka wa Msumbiji na Tanzania.

Wanamagambo katika mji wa Palma, kaskazini mwa Msumbiji

Mji wa Palma ulio karibu na mradi mkubwa ya gesi wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 60 na ambao ni makao makuu ya kampuni kadhaa za kigeni ulilengwa na mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha tarehe 24 mwezi Machi mwaka huu.

Makumi ya raia waliuawa na wengine wasiopungua 11,000 walikimbia makazi yao baada ya wanamgambo wenye mfungamano na ISIS (Daesh) kuuvamia na kuuteka mji huo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi.  

Tags