Apr 12, 2021 02:51 UTC
  • Wapiganaji wa kundi la Daesh, Msumbiji
    Wapiganaji wa kundi la Daesh, Msumbiji

Katika miaka ya hivi karibuni makundi ya kigaidi yameimarisha harakati zao katika nchi mbalimbali za Kiafrika. Genge la Daesh ni miongoni wa makundi hayo ya kigaidi ambayo yamezidisha mashambulizi na harakati zao katika nchi za Afrika.

Wiki kadhaa zilizopita kundi hilo lilivamia na kuteka mji wa pwani wa Palma huko Kaskazini mwa Msumbiji na kuua makumi ya watu. Kundi hilo pia limefanya uharibifu katika miji mingine mitatu ya Msumbiji.

Kasi ya kukua na kusambaa kundi hilo la kigaidi la Daesh imewatia wasiwasi maafisa usalama Msumbiji na nchi kadhaa za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika. Kwa sababu hiyo siku chache zilizopita ulifanyika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama wa nchi za jumuiya hiyo huko Maputo nchini Msumbiji. Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni masuala ya usalama na hatua za kukabiliana na vitendo vya ugaidi katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

Mkutano wa SADC, Msumbiji

Kwa miaka kadhaa sasa baadhi ya nchi za Kiafrika zimekuwa uwanja wa harakati za makundi ya kigaidi. Harakati za makundi hayo zimeshadidi zaidi katika miaka ya karibuni kutokana na kuungana kwa baadhi ya makundi ya waasi na makundi ya kigaidi kama Boko Haram na Daesh na kushadidi hitilafu ndani ya makundi ya kigaidi yenyewe. 

Kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria na machafuko yanayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika kama Libya, Niger, Kaskazini mwa Mali na Somalia na utajiri wa maliasili unaopatikana katika nchi nyingi za bara hilo vimeandaa mazingira mazuri kwa makundi mengi ya kigaidi yaliyokuwa Iraq na Syria kukimbia Afrika.

Taqi al Najjar ambaye ni mtafiti wa Kituo cha Uchunguzi wa Kistratijia cha Misri anasema: "Baada ya kupoteza ngome na kambi zao huko Iraq na Syria magaidi wa kundi la Daesh waliamua kuelekea barani Afrika kutokana na nchi za bara hilo kuwa na mazingira yanayoruhusu harakati za kigaidi la kundi hilo." 

Wapiganaji wa kundi la Daesh

Mashambulizi ya kundi la Daesh katika mji wa Palma huko Kaskazini mwa Msumbiji yanatambulia kuwa ni kengele ya hatari kwa nchi nyingine za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika. Kundi hilo limekuwa likitumia mbinu za kikatili na za kutisha kama kukatwa vichwa vya raia kwa shabaha ya kupanua mamlaka na udhibiti wao katika nchi hiyo ya Kiafrika. Mji wa Palma uko karibu na mradi mkubwa ya gesi na ni makao ya kampuni kadhaa za kigeni ikiwemo ile ya Total la Ufaransa. Kabla ya mapatano ya sasa ya Libya pia kundi hilo la Daesh lilivamia na kuteka visima vya mafuta na gesi huko Libya. Inaonekana kuwa, wapiganaji wa kundi hilo wanalenga maeneo hayo kwa shabaha ya kudhamini kipato cha kuendeshea shughuli na harakati za kigaidi katika maeneo mengine ya dunia.

Hali hii inashuhudiwa katika nchi za Afrika licha ya madola makubwa ya Magharibi kudai kuwa yako mstari wa mbele kusaidia nchi hizo katika mapambano dhidi ya ugaidi. Si hayo tu, bali baadhi ya nchi za Magharibi kama Ufaransa na Marekani zimetuma majeshi yako huko Afrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi lakini kinyume chake harakati za kigaidi zimeendelea kupanuka zaidi siku baada ya nyingine barani humo. Nchi hizo za Magharibi zinatumia kisingizio hicho kwa ajili ya kuimarisha uwepo wao barani Afrika na kuingilia masuala ya ndani ya nchi za bara hilo. Kama mfano tu, siku chache zilizopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Augusto Santos Silva ametangaza kuwa nchi yake itatuma wanajeshi 60 nchini Msumbiji kwa shabaha ya kukabiliana na wapiganaji wa kundi la Daesh. Msumbiji ni miongoni mwa makoloni ya zamani ya Ureno. Vilevile msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, John Francis Kirby amedai kuwa, nchi hiyo itaisaidia Msumbiji kukabiliana na ugaidi na makundi yenye misiamo ya kufurutu ada.

Raia wa mji wa Palma ulioshambuliwa na Daesh

Inaonekana kuwa, mbali na matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama yanayosababishwa na harakati za makundi ya kigaidi na ya waasi, Afrika pia inazongwa na harakati haribifu za nchi za Magharibi zainazoendelea kumimina majeshi yao katika nchi za bara hilo kwa kutumia visingizio bandia ikiwa ni pamoja na madai ya kupambana na ugaidi. Kuwepo kwa majeshi ya wakoloni hao wa zamani barani Afrika kunatishia uhuru na mamlaka ya kujitawala ya nchi za bara hilo.      

Tags