May 29, 2021 14:10 UTC
  • Kukiri Ujerumani kwamba ilihusika na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Namibia, ushahidi mwingine wa jinai dhidi ya binadamu za nchi za Magharibi

Kwa mara ya kwanza kabisa Ujerumani imekiri kwamba, ilifanya mauaji ya kimbari dhidi watu wa Namibia katika kipindi cha ukoloni wa nchi hiyo barani Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Heiko Maas ametoa taarifa akitangaza kuwa, Berlin inatambua rasmi matukio yanayotajwa kuwa ni mauaji ya kimbari nchini Namibia. Heiko Maas amesema, chini ya kivuli cha kukubali majukumu yake ya kihistoria na kimaadili, Ujerumani inaiomba msamaha Namibia na familia za wahanga wa ukatili uliofanyika nchini humo. 

Wakoloni wa Ujerumani waliua kwa umati makumi ya maelfu ya watu wa makabila ya Herero na Nama kwenye mauaji ya kuangamiza kizazi yaliyotokea baina ya mwaka 1904 na 1908 ambayo wanahistoria wanayataja kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20. Mauaji makubwa yaliyofanywa na Wajerumani na vilevile kitendo cha wakoloni hao cha kuwafukuza wanawake na watoto wadogo na kuwapeleka maeneo ya mbali majangwani kilisababisha vifo vya maelfu ya watu wa Namibia waliopoteza maisha kutokana na kiu na njaa. Wakoloni hao wa Kijerumani pia walijenga kambi za kuwatumikisha kwa nguvu raia wa Namibia. Wakati wa mapigano ya Waterberg (Battle of Waterberg) Agosti mwaka 1904, karibu watu elfu 80 wa kabila la Herero wakiwemo wanawake na watoto, walikimbia nyumba na makazi yao na kukimbizwa na wanajeshi wa Ujerumani hadi kwenye Jangwa la Kalahari. Nyaraka za historia zinaonesha kuwa, watu elfu 15 miongoni mwao tu ndio walionusurika. Jinai hiyo ya Wajerumani inayotajwa na wanahistoria kuwa ndiyo mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20, ilivuruga uhusiano wa Namibia na Ujerumani kwa miaka mingi. Japokuwa Ujerumani ilikuwa imekubali kwamba, wanajeshi wake walifanya ukatili nchini Namibia mwanzoni mwa karne ya 20 lakini ilikuwa imekataa kulipa fidia ya jinai hiyo. 

Wananchi wa Namibia waliokufa kwa njaa na kiu majangwani kwa ukatili wa Ujerumani 

Katika kipindi cha karne kadhaa za ukoloni wao barani Afrika wazungu wa Ulaya waliwafanya watumwa watu weusi wa bara hilo kwa kuwasafirisha hadi kwenye makoloni yao mengine ya America na Kaskazini, America ya Latini na maeneo mengine ya dunia ambako waliwatumikisha kwenye kazi za sulubu na mashamba yao. Vilevile wazungu hao walipeleka Afrika magonjwa yaliyokuwa yameenea barani Ulaya  na kuwatumbukiza maelfu ya Wafrika katika makucha ya mauti. 

Jinai za wazungu wa Ulaya barani Afrika hazikuishia hapo, bali wakoloni hao walitenda ukatili wa kutisha katika maeneo mbalimbai ya bara hilo. Miongoni mwa jinai za wakoloni hao ni zile zilizofanywa na wanajeshi wa Ufaransa katika makoloni ya nchi hiyo barani Afrika na mauaji ya kutisha ya wanajeshi wa Ubelgiji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mwaka 1891 Wabelgiji  walihodhi uzalishaji wa zao la mpira na meno ya tembo nchini Congo na wakaanzisha mfumo wa kikatili kupita kiasi uliowalazimisha watu wa nchi hiyo kufanya kazi za kulazimishwa. Katika kitabu chake alichokipa jina la "Kunyesha kwa Mvua ya Mkono Juu ya Congo", Marc Wiltz anasema: "Kuna uwezekano kwamba katika kipindi cha miaka 23 karibu Wacongo milioni kumi, yaani zaidi ya thuluthi moja ya jamii yote ya nchi hiyo, waliuawa na wakoloni."

Marc Wiltz

Jinai na mauaji ya wakoloni hao yaliendelea katika karne ya 20 na sambamba na vita vya kupigania uhuru kwenye nchi za Afrika hususan baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Miongoni mwa mauaji hayo ni yale yaliyofanywa na wanajeshi wa Uingereza dhidi ya wapiganaji wa Mau Mau nchini Kenya kati ya miaka ya 1952 na 1960. 

Ufaransa pia ambayo iliikoloni Algeria ilifanya jinai na mauaji ya kutisha katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wakati wa mapambano ya kupigania uhuru ya wazalendo wa nchi hiyo. Waalgeria milioni moja waliuawa na wakoloni wa kifaransa. Licha ya Ufaransa kukiri kwamba ilitendeka jinai hiyo lakini hadi sasa imekataa kuwaomba radhi watu wa Algeria.

Katika karne hii ya 21 pia Ufaransa ilishiriki katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyochukua roho za watu milioni moja. Matokeo ya uchunguzi uliofanyika mwaka 2017 kwa maagizo ya serikali ya Rwanda yalibaini kuwa, serikali ya Ufaransa ilishirikiana na Wahutu wenye misimamo mikali katika mauaji ya Watutsi zaidi ya laki nane. Uchunguzi huo uliokusanywa kwenye kurasa karibu mia sita unasisitiza kuwa, Ufaransa ilikuwa na taarifa kamili kuhusu mipango ya mauaji ya kimbari ya Rwanda. 

Hatua ya sasa ya Ujerumani ya kukiri kwamba ilifanya mauaji ya kimbari nchini Namibia inaonesha kuwa, licha ya madai ya kutetea haki za binadamu na propaganda zao za kupigania huru, heshima na hadhi ya mwanadamu lakini historia ya ukoloni wa nchi za Magharibi inakadhibisha kabisa madai hayo.    

Tags