Jun 06, 2021 02:34 UTC
  • Makumi wauawa katika shambulio la watu wenye silaha Burkina Faso

Watu waliokuwa na silaha wasiojulikana wameshambulia kijiji kimoja kaskazini mwa Burkina Faso na kuua makumi ya raia.

Shirika la habari la Reuters limenukuu duru za kiusalama zikiripoti kuwa, takriban watu 100 wameuawa katika hujuma hiyo ya usiku wa kuamkia jana Jumamosi katika kijiji cha Solhan mkoani Yagha, mpakani mwa nchi hiyo na Niger.

Habari zinasema kuwa, wabeba silaha hao walikivamia kijiji hicho na kutekeleza ukatili huo, mbali na kuteketeza moto nyumba na soko la kijiji hicho kabla ya kutoroka masaa kadhaa baadaye.

Serikali ya nchi hiyo kupitia Rais Marc Christian Kabore imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia jana usiku kufuatia mauaji hayo ya kutisha. 

Awali shirika la habari la Sputnik lilikuwa limeripoti kuwa, waliouawa katika shambulio hilo ni watu wasiopungua 11, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Maafisa usalama wametumwa katika kijiji hicho kwenda kulinda doria na kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.

Maafisa usalama wa Burkinabe wakiwasaka wabeba bunduki kaskazini mwa nchi

Mapema mwezi uliopita wa Mei, watu wasiopungua 32 waliuawa na wengine 17 walijeruhiwa katika shambulio jingine la wabeba silaha kaskazini mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Katika miaka ya karibuni, Burkina Faso imekumbwa mara kadhaa na hujuma za mashambulio ya umwagaji damu. Mashambulio hayo kwanza yalianzia kaskazini na baadaye yakaenea hadi mashariki na katikati ya nchi hiyo. Mashambulio ya kigaidi ambayo yameshuhudiwa nchini Burkina Faso kuanzia mwaka 2015 hadi sasa yameshapelekea mamia ya watu kuuawa. Aghalabu ya mashambulio hayo yametokea kwenye maeneo ya mipaka ya pamoja ya nchi hiyo na Mali, Niger na Benin.

 

Tags