Jun 10, 2021 02:32 UTC
  • Magaidi wanawateka nyara watoto nchini Msumbiji

Mwakilishi wa Taasisi ya Kulinda Watoto nchini Msumbiji imeripoti kuwa, magaidi nchini humo wanawateka nyara watoto.

Chance Briggs, mwakilishi wa taasisi hiyo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Mataifa, kitendo cha kuwateka nyara watoto ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto katika mizozo na migogoro ya kivita.

Naye Paula Sengo, Mshauri Anayehusika na Ulinzi wa Watoto katika Taasisi hiyo ya Msumbuji amesema kuwa, vitendo vya ukiukaji wa haki za watoto vimeongezeka sana nchini humo. Jumla ya watoto 51 wametekwa nyara katika mashambulizi ya makundi ya kigaidi kaskazini mwa Msumbuji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na maelfu ya watu wameuawa.

Mkoa tajiri wa gesi wa Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji 

Hii ni katika hali ambayo taasisi za kiraia za nchini Msumbiji zimeitaja idadi ya watoto waliotekwa nyara na makundi ya kigaidi nchini humo hadi sasa kuwa zaidi ya hiyo iliyotajwa. Makundi ya kigaidi yalianza kuwateka nyara watoto huko Msumbiji tangu mwaka jana, 2020.  

Mapema mwaka huu Shirika la Save the Children liliripoti kuwa, watoto wenye umri wa miaka isiyopungua 11 wanalengwa na machafuko na mashambulizi ya magaidi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kisha kuuawa. Shirika hilo lilisema kuwa, linasikitishwa na ripoti zinazoeleza kwamba magaidi wanalenga watoto katika hujuma zao huko katika mkoa tajiri kwa gesi wa Cabo Delgado. 

Tags