Jun 24, 2021 07:24 UTC
  • SADC yaafiki mpango wa kutuma wanajeshi nchini Msumbiji

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC zimeafikiana juu ya mpango wa kutuma wanajeshi nchini Msumbiji kuisaidia Maputo kupambana na magenge ya magaidi na waasi huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Stergomena Tax, Katibu Mkuu wa SADC baada ya kufanyika mkutano wa siku moja wa jumuiya hiyo katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, ambapo amebainisha kuwa, nchi wanachama wa jumuiya hiyo zimekubaliana juu ya kutumwa wanajeshi katika mkoa wa Cabo Delgado, huko kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, kwenda kusaidia kuzima harakati za ugaidi na uasi.

Hata hivyo taarifa ya mwisho ya mkutano wa jumuiya ya SADC haijafafanua idadi ya askari wanakaotumwa, muda watakaotumwa na majukumu yao huko Msumbiji yatakuwa yapi.

Katika mkutano wa mwezi Mei mwaka huu, jumuiya hiyo ya kikanda ilisimamisha mpango huo wa kutuma wanajeshi Msumbiji, na badala yake ikasema itaisaidia Maputo kwa njia nyingine kupambana na uasi unaohatarisha usalama wa eneo hilo zima.

Wakati huo, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji alisisitiza kuwa, nchi yake inabidi itatue yenyewe jambo hilo na haitoruhusu uingiliaji wa kigeni wa kijeshi kwani lazima iweze kulinda uhuru wake wa kujitawala.

Nembo ya SADC

Machi mwaka huu, waasi waliuteka mji wa Palma wa kaskazini mwa Msumbiji katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania, na kuua makumi ya watu na kuwalazimisha kuwa wakimbizi watu wengine zaidi ya 50,000. Eneo hilo limekumbwa na uasi baada ya kuanza mradi wa gesi wa dola bilioni 20.

Watu zaidi ya elfu tatu wameuawa, huku wengine zaidi ya laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika mkoa wa Cabo Delgado tokea mwaka 2017.

Tags