Jun 30, 2021 11:02 UTC
  • Somalia yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais

Baada ya kushuhudiwa miezi kadhaa ya mkwamo wa kisiasa nchini Somalia, hatimaye viongozi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wameafikiana kuhusu tarehe ya kufanyika uchaguzi usio wa moja kwa moja wa rais.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Somalia, Mohamed Hussein Roble katika taarifa na kuongeza kuwa, uchaguzi huo wa rais na bunge ambao umesubiriwa kwa muda mrefu, sasa utafanyika Oktoba 10.

Amesema wadau wote wa kisiasa nchini humo wameafikiana juu ya ramani ya njia ya kufanyika zoezi hilo la kidemokrasia, baada ya kufanyika mkutano wa siku mbili katika mji mkuu Mogadishu.

Waziri Mkuu wa Somalia amewapongeza viongozi wa nchi hiyo baada ya mazungumzo hayo kuzaa matunda, huku akisisitiza kuwa anatumai uchaguzi huo utakuwa huru, wa haki, ulio wazi na wa amani.

Itakumbukwa kuwa, Serikali Kuu na viongozi wa majimbo matano ya Somalia walishindwa kukubaliana kuhusu masharti ya upigaji kura, mivutano ambayo iliendelea hadi muda wa kufanyika uchaguzi yaani mwezi Februari mwaka huu, ukapita na Rais Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kwa jina la Farmajo akaongezewa muda wa urais wake kwa miaka miwili na Bunge la nchi hiyo.

Rais Farmajo

Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Mei, wabunge wa Somalia walipiga kura na kubatilisha uamuzi wao wa awali wa kumuongezea muda wa kubakia madarakani rais huyo.  Bunge la Somalia lilichukua hatua hiyo baada ya kuzuka mivutano na mzozo mkubwa nchini humo.

Baada ya kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje ya nchi, Rais Farmajo alibatilisha uamuzi wake na kutangaza kuwa hataongeza muhula wake madarakani kwa muda wa miaka miwili. 

Tags