Jul 03, 2021 12:40 UTC
  • Watu 10 wauawa baada ya gaidi kujiripua Mogadishu, Somalia

Kwa akali watu kumi wameuawa baada ya gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu kujiripua katika mkahawa mmoja wenye shughuli nyingi kwenye makutano ya barabara ya Jubba, katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutaja jina lake amenukuliwa na shirika la habari la Xinhua akisema kuwa, mbali na watu kumi kuuawa kwenye mripuko huo mkahawani katika wilaya ya Shibis, wengine wasiopungua tisa wamejeruhiwa.

Amesema yumkini idadi ya wahanga wa shambulio hilo linalosadikika kuwa la kigaidi ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya baadhi ya majeruhi wa hujuma hiyo. 

Ahmed Abdi, mmoja wa mashuhuda amesema mripuko huo umeharibu majengo kadhaa yanayopakana na hoteli iliyoripuliwa kwenye shambulio hilo la jana Ijumaa. Hadi tunamaliza kuandaa taarifa hii, hakuna genge lililokuwa limetangaza kuhusika na shambulio hilo.

Majeruhi wakiwahishwa katika vituo vya afya

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu 12 kuuawa kufuatia mashambulio mawili ya kigaidi yaliyolenga kituo kimoja cha kijeshi na eneo la makazi ya raia katika jimbo la Galmudug, katikati mwa Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilitoa taarifa likitangaza kuhusika na mashambulio hayo ambayo limedai yaliua askari 32 wa serikali kuu na ya kieneo. Kundi hilo la kigaidi ambalo liliasisiwa mwaka 2004 lina fikra potovu ambazo zinahusishwa na kundi jingine la kigaidi la al-Qaida.

 

Tags