Jul 05, 2021 10:19 UTC
  • Algeria: Ufaransa inakataa kutoa ramani ya maeneo yaliyotumiwa kwa majaribio ya nyuklia

Waziri wa Mujahideen (maveterani wa vita vya ukombozi) nchini Algeria, Tayeb Zitouni amesema kuwa Ufaransa inakataa kuikabidhi nchi hiyo ramani ya maeneno yaliyotumiwa kwa ajili ya majaribio ya milipuko ya nyuklia yaliyofanywa na serikali ya Paris katika majangwa ya Algeria kwenye miaka ya sitini ya karne iliyopita.

Waziri wa Maveterani wa Vita vya Ukombozi wa Algeria ameyasema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa mkoloni Mfaransa miaka 59 iliyopita. Zitouni amesema Ufaransa inakataa kuikabidhi Algeria ramani za maeneo hayo ambazo zinaweza kusaidia kujua maeneo zilikozikwa taka na sumu na kemikali za nyuklia ambazo hazijagunduliwa hadi hivi sasa.

Waziri wa Maveterani wa Vita vya Ukombozi wa Algeria ameongeza kuwa, hadi sasa Ufaransa haijachukua hatua yoyote ya kusafisha maeneo hayo yenye taka za nyuklia au kuchukua hatua yoyote ya kibinadamu ya kuwafidia watu waliopatwa na maafa kutokana na mjaribio ya nyuklia ya nchi hiyo katika ardhi ya Algeria.

Amesema kuwa, milipuko ya nyuklia iliyofanywa na Ufaransa nchini Algeria wakati wa ukoloni ni ushahidi wa kutosha wa jinai kubwa zilizofanywa na Paris ambazo athari zake mbaya zingali zinawaumiza watu na mazingira.a

Algeria

Wanahistoria wanasema utawala wa kikoloni wa Ufaransa ulifanya majaribio kadhaa ya nyuklia katika jangwa la Algeria, 4 juu ya ardhi na 13 chini ya ardhi, kati ya 1960-1966.

Ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria uliendelea katika kipindi cha kati ya 1830 na 1962, na maafisa wa Algeria na wanahistoria wanasema kwamba, kipindi hicho kilishuhudia mauaji dhidi ya watu karibu milioni 5, sambamba na kampeni za kuhamishwa mamilioni ya wengine na kuporwa utajiri na mali ya taifa hilo.

Tags