Jul 13, 2021 10:06 UTC
  • Umoja wa Ulaya kutoa mafunzo kwa jeshi Msumbiji ili kupambana na Daesh

Umoja wa Ulaya umeanzisha rasmi kampeni ya kijeshi ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya ulinzi vya Msumbiji vinavyopambana na wanamgambo wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh huko katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Jimbo tajiri kwa nishati ya gesi la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na machafuko na hujuma za wanamgambo wenye mfungamano na Daesh tangu mwishoni mwa mwaka 2017. Hadi sasa watu wasiopungua 3,000 wameuliuwa katika hujuma za wanamgambo hao na wengine laki nane wamelazimika kuhama makazi yao. Tayari Ureno, nchi mkoloni wa zamani wa Msumbiji, inatoa mafunzo kwa jeshi la Msumbiji. 

Jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji 

Wakufunzi wa kijeshi wa Ureno nchini Msumbiji wanatarajiwa kuunda nusu ya ujumbe mpya wa EU, ambao utaongozwa na kamanda wa Ureno.

Taarifa ya EU imeeleza kuwa, ujumbe huo wa kijeshi utatoa mafunzo na kulisaidia jeshi la Msumbiji kuwaliwanda raia na kudumisha amani na usalama katika jimbo la Cabo Delgado. Ujumbe huo utabakia nchini Msumbiji kwa kipindi cha miaka miwili. Ukiwa nchini Msumbiji, ujumbe huo wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya utasaidia kuvijengea uwezo vikosi vya ulinzi vya Msumbiji  ambavyo vitakuwa sehemu ya kikosi cha radiamali ya haraka. 

Mwezi Juni mwaka huu, mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa, nchi nyingine zikiwemo Ufaransa, Italia na Uhispania pia zinatazamiwa kutuma wanajeshi kujiunga na timu hiyo ya Umoja wa Ulaya. 

Mwezi uliopita pia nchi 16 wanachama katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ziliidhinisha kutumwa wanajeshi huko Msumbiji baada ya serikali ya Maputo kusema kuwa inakaribisha wanajeshi kutoka mataifa mengine ili kusaidia mapambano dhidi ya wanamgambo hao. 

Rwanda nayo Ijumaa iliyopita ilitangaza kuwa, itatuma askari jeshi na polisi wapatao elfu moja katika jimbo lililoathiriwa na machafuko la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji. 

Tags