Jul 25, 2021 08:26 UTC
  • Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuenea ugaidi barani Afrika

Katika ripoti yao mpya, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa bara la Afrika limekuwa muhanga mkuu wa ugaidi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 kutokana na kuenea makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaida na makund mengine yaliyo chini ya udhibiti na ushawishi wa makundi hayo mawili.

Ujumbe wa wataalamu hao uliowasilisha ripoti hiyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Ijumaa, unasema kwamba makundi hayo ya kigaidi yameeneza shughuli zao katika maeneo ya magharibi na mashariki mwa Afrika ambapo yana uwezo mkubwa wa kujidhaminia fedha na kutumia silaha za kisasa ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kigaidi. Wanasema matawi yanayofungamana na makundi hayo mawili makuu ya ugaidi yamejizatiti katika maeneo ya Afrika ya Kati, Sahel, magharibi na mashariki kwa Afrika na hasa nchini Somalia ambayo kwa sasa haina serikali kuu yenye nguvu.

Ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuenea makundi ya kigaidi barani Afrika kwa hakika inaweka wazi ongezeka kubwa la shughuli za makundi ya kigaidi katika bara hilo na hasa eneo la Sahel, ambalo limekuwa uwanja na maficho makuu ya makundi ya Daesh na al-Qaida pamoja na matawi yake barani humo.

Katika kipindi cha miaka 6 iliyopita, mashambulio ya makundi hayo yameongezeka karibu mara 20 na wahanga wake mara 9 zaidi.

Baadhi ya makundi ya magaidi Afrika Magharibi

Suala la kuongezeka ugaidi na misimamo ya kupindukia mipaka katika eneo la Sahel limetokea kuwa tatizo kubwa katika eneo hilo kwa kadiri kwamba ni miaka mingi sasa ambapo majeshi na polisi ya nchi za eneo hilo na hasa Mali, Niger na Burkina Faso yamekuwa yakitumia fedha na muda wao mwingi kupambana na makundi hayo.

Kuna sababu kadhaa tofauti ambazo zimechangia tatizo hilo. Moja ya sababu hizo ni kuwa eneo hilo lina mambo mengi yanayochangia vijana kujiunga na makundi ya kigaidi. Kwa kawaida vijana hao masikini huwa kwenye hali mbaya ya kimaisha na hivyo huathirika haraka na nara za hadaa za kutajirika haraka, zinazotolewa na makundi ya kigaidi.

Sababu nyingine ni kutokuwepo maendeleo ya kitosha kiuchumi, kijamii na kimiundomsingi katika nchi nyingi za Afrika na hasa zile zilizopo katika eneo la Sahel. Sababu hiyo imepelekea vijana wengi kuhatarisha maisha yao kwa kuamua kusafiri kimagendo kuelekea nchi za Ulaya kupitia nchi za kaskazini mwa Afrika, hasa Libya. Kukataa tamaa maishani kumewafanya vijana wengi katika nchi hizo kushawishiwa kirahisi na makundi ya kigaidi na hivyo kubeba silaha dhidi ya raia na serikali zao dhaifu na hatimaye kuharibu zaidi hali ya mambo katika nchi hizo.

Wataalamu wa Umoja wa Matifa wanasema, kuenea kwa makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel na hasa katika nchi za Mali, Burkina Faso, Ivory Coast, Niger, Senegal, Nigeria, Chad na Cameroon kumeongeza wasi wasi na hofu kubwa katika nchi hizo. Wanasema makundi yanayofungamana na Daesh na al-Qaida sasa yameimarisha shughuli zao katika eneo la mashariki mwa Afrika tokea Somali hadi Kenya na Tanzania hadi Msumbiji.

Suala ambalo limezua wasi wasi kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi barani Afrika ni uwepo barani humo wa nchi za Magharibi na hasa Ufaransa na Marekani kwa madai ya kupambana na ugaidi. Licha ya kuwa Ufaransa ilituma askari wake huko Mali miaka minane iliyopita kwa kisingizio cha kupambana na tishio la makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaida lakini Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo alisema siku chache zilizopita kwamba nchi yake sasa imeamua kusitisha operesheni hiyo na kwamba itapunguza idadi ya askari wake walioko nchini humo ambao wanafikia elfu 5 hadi nusu.

Uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa magharibi mwa Afrika

Licha ya miaka mingi ya madai ya kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel, Ufaransa si tu kwamba haijapata mafanikio yoyote katika uwanja huo bali imechochea zaidi shughuli za makundi hayo katika eneo hilo. Nchi hiyo sasa inaitika Marekani itume askari wake katika eneo hilo kwa kisingizio cha kupambana na magaidi. Pamoja na hayo ni wazi kuwa makundi ya kigaidi yanaendelea kuongeza shughuli na wanachama wao barani Afrika na hasa katika eneo la Sahel.

Jordan Koop, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anaashiria shughuli za makundi ya kigaidi barani Afrika na hali mbaya ya bara hilo katika nyanja za uchumi, siasa na usalama na kusema: Katika siku zijazo kutatokea vita vikubwa dhidi ya ugaidi na wala ASia Magharibi hakitakuwa tena kitovu muhimu cha mapambano dhidi ya fikra na mielekeo ya kupindukia mipaka.

Tags