Aug 01, 2021 08:04 UTC
  • UN: Raia sita wauawa katika shambulio la waasi kaskazini mwa CAR

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu sita wameuawa katika shambulio la waasi wanaobeba silaha kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Msemaji wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (Minusca) amesema watu hao waliuawa jana Jumamosi baada ya watu waliobeba silaha wa genge la 3R (Return, Reclamation, Rehabilitation) kushambulia kijiji cha Mann, kaskazini mashariki mwa nchi.

Amesema mbali na watu sita kuuawa katika hujuma hiyo, wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Luteni Kanali Abdoulaziz Fall ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hali sasa hivi ni shwari katika kijiji hicho kilichoko umbali wa kilomita 550 kutoka mji mkuu, Bangui na kwamba maafisa usalama wanalinda doria.

Ramani ya CAR

Wakazi wa kijiji hicho wanasema wanachama wa kundi la 3R linalodai kupigania maslahi ya jamii ya Fulani waliingia kijijini hapo na kuanza kufyatua risasi ovyo na kuua watu sita na kujeruhi wengine wengi.

Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa madini imekuwa katika mgogoro na mapigano ya kidini na kikabila tokea mwaka 2013. 

Tags