Aug 02, 2021 04:19 UTC
  • Rais wa Zambia aliamuru jeshi kukabiliana na ghasia za kuelekea uchaguzi mkuu

Rais Edgar Lungu wa Zambia ametoa agizo na kulitaka jeshi, kikosi cha anga na kikosi cha usalama wa taifa kuisaidia polisi katika kudhibiti ghasia zinazoshuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ili kuzuia kuvuruga utaratibu wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 12.

Rais wa Zambia amesema kuuwa, kudumisha utekelezaji wa sheria na utulivu ni kazi ya kila siku ya polisi, lakini baadhi ya wakati wanahitaji msaada kutoka vitengo vingine vya usalama.

Rais Edgar Lungu amesisitiza kuwa, amechukua hatua hiyo ili kuhakikisha kwamba, uchaguzi ujao unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na uhuru kamili. Hata hivyo hatua hiyo imekosolewa na kulalamikiwa na wapinzani.

Kwa mujibu wa rais Lungu vikosi vya usalama vimesambazwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Lusaka, ambao umeshuhudia ghasia katika siku mbili zilizopita na kusababisha vifo vya watu wawili, na kuongeza kwamba, maofisa wengine watapelekwa katika sehemu nyingine za nchi kama hali itaruhusu.

Rais Edgar Lungu wa Zambia

 

Taarifa za awali zinasema kuwa, watu wawili waliouawa ni wafuasi wa chama tawala na inasemekana kuwa, huenda waliuawa na wafuasi wa mrengo wa upinzani. Watu wanne wametiwa mbaroni wakihushwa na mauaji hayo.

Wakati huo huo, Tume ya Uchaguzi ya Zambia imepiga marufuku mikkusanyiko ya kampeni za uchaguzi kutokana na kuenea virusi vya corona. Edgar Lungu (64) anagombea tena kwa kipindi cha pili ambapo anapewa nafasi kubwa ya kuibuka na uushindi katika uchaguzi huo wa tarehe 12 mwezi huu.