Aug 03, 2021 12:15 UTC
  • Makumi ya maiti zapatikana kwenye mto ulioko mpakani mwa eneo la Ethiopia la Tigray na Sudan

Maiti zisizopungua 30 zilizosombwa na maji zimepatikana kwenye kingo za mto unaotenganisha Sudan na eneo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray. Hayo ni kwa mujibu wa wakimbizi wawili wa Ethiopia na mashuhuda wanne raia wa Sudan waliookota maiti hizo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, maiti hizo zimepatikana kwenye fukwe za Mto Setit, unaojulikana nchini Ethiopia kwa jina la Tekeze, ambao unapita kwenye mpaka wa pamoja wa Ethiopia na Eritrea kabla ya kuvuka na kuingia Sudan kwenye nukta ya mpaka inayozikutanisha nchi hizo tatu.

Dakta Tewodros Tefera, bingwa wa upasuaji aliyetorokea Sudan kutoka mji wa mpakani mwa Ethiopia wa Humera ameyaeleza mashirika ya habari kuwa, katika muda wa siku sita zilizopita alizika maiti kumi ndani ya ardhi ya Sudan; na alielezwa na wavuvi na wakimbizi kwamba maiti nyingine 28 zimepatikana, zikiwemo saba zilizookotwa jana Jumatatu.

Kwa mujibu wa daktari huyo maiti hizo ni za watu waliopigwa risasi vifuani, tumboni na miguuni huku mikono yao ikiwa imefungwa. Ameongeza kuwa kwa msaada wa wakimbizi aliweza kuzitambua maiti tatu kuwa ni za Watigray kutoka mji wa Humera. Watigray wengi kutoka mji huo walikimbilia nchi jirani ya Sudan wakati yalipoanza mapigano kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF.

Wapiganaji wa harakati ya TPLF

Maafisa wawili wa Sudan pamoja na raia wawili wakazi wa mji kilipo kijiji cha Wadd al-Hilew karibu na bwawa la Setit katika jimbo la Kassala wamesema waliopoa maiti 20 kutoka kwenye Mto Setit; sita siku ya Jumamosi, tisa Jumapili na maiti nyingine tano Jumatatu ya jana.

Maafisa wa serikali ya Ethiopia wamekataa kueleza chochote kuhusu ripoti hizo pamoja na filamu za video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha miili ya watu hao iliyookotwa kwenye kingo za Mto Setit. Akaunti rasmi ya Twitter ya serikali ya Addis Ababa imebeza ripoti na picha hizo ikisema, zinatokana na kampeni bandia zinazoendeshwa na "wafanyapropaganda" wa Tigray.../

 

Tags