Dec 12, 2020 11:23 UTC
  • Amir-Abdollahian: Kama watawala wa Kiarabu wameghafilika na Uislamu basi wafikirie japo maana ya ‘ghera ya Kiarabu’

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, hatua ya Morocco ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni usaliti na pigo la jambia dhidi ya mwili wa muqawama wa Palestina.

Hussein Amir-Abdollahian amebainisha kwamba, baadhi ya watawala wa ulimwengu wa Kiarabu kama wameghafilika na Uislamu asili wa Mtume Muhammad SAW, basi kwa uchache watafakari kuhusiana na maana ya ‘ghera ya Kiarabu’.

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesisitiza kuwa, hapana shaka yoyote kwamba, Wazayuni hawana nafasi yoyote katika mutakbali wa eneo la Asia Magharibi.

Alkhamisi iliyopita mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa, amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

 

Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. 

Itakumbukwa kuwa, tarehe 25 Septemba mwaka huu, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Sudan pia tayari imefuata mkumbo huo huo na kutangaza utayarifu wa kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia.

Tags