Jan 04, 2021 11:03 UTC
  • Kukosoa ripota wa Umoja wa Mataifa hatua isiyo ya kisheria ya Marekani ya kumuua Qassim Suleimani

Januari 3 mwaka uliomalizika hivi majuzi wa 2020, kwa amri ya Rais Donald Trump, utawala wa kigaidi wa Marekani ulifanya jinai ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani, Mkuu wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashd al-Shaabi katika shambulio la anga lililofanywa jirani na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.

Aidha wanamapambano wengine wanane waliokuwa wameandamana na makamanda hao wa muqawama nao waliuawa shahidi katika shambulio hilo.  

Mauaji hayo ya kinyama yalilaaniwa na kabiliwa na ukosoaji mkubwa kieneo na hata katika uga wa kimataifa. Bi Agnès Callamard, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Jumapili ya jana tarehe 3 Januari aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Mauaji dhidi ya Qassim Suleimani yalikinzana wazi na vigezo vya kimataifa vya haki za binadamu.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema bayana kuwa, madai ya Marekani kwamba Luteni Jenerali Suleimani alikuwa tishio kwa usalama wa roho za Wamarekani huko Iraq hayana msingi wowote, na hivyo kumuua jenerali huyo kulikanyaga na kukiuka sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa.

Mashahidi Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis

 

Sisitizo la ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena katika wakati huu wa hauli na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimni ni ishara ya wazi ya umuhimu wa kadhia hii hususan kwa kuzingatia ukiukaji wa haki za binadamu na vigezo vya kimataifa.

Kisingizio cha Trump ambaye uongozi wake umo katika siku za mwisho za uhai wake katika Ikulu ya White House cha kutekeleza jinai hiyo ni madai kwamba, eti Luteni Jenerali Qassim Suleimani alielekea Iraq kwa minajili ya kutekeleza mipango ya mashambulio dhidi ya Wamarekani na vituo vyao vya kijeshi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Hii ni katika hali ambayo, madai haya yasiyo na maana yamepingwa hata na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani. Ukweli wa mambo ni kuwa, nyaraka mbalimbali na matamshi ya viongozi wa Marekani yanaonyesha kuwa, miezi kadhaa nyuma Washington ilikuwa imeshachukua uamuzi wa kumuua Luteni Jenerali Qassim Suleimani na ilichokuwa inasubiri ni wakati mwafaka tu wa kutekeleza hatua hiyo ya kijinai.

Rais Donald Trump wa Marekani 

 

Kanali ya Televisheni ya NBC ya Marekani Januari 13 mwaka jana (2020) ilitangaza ripoti inayoonyesha kwamba, Juni mwaka 2019, yaani miezi saba kabla, Trump alishatoa agizo lenye masharti la kuuliwa Luteni Jenerali Qassim Suleimani.

Kwa mtazamo wa washauri wa masuala ya kijeshi na kiusalama wa Trump ni kuwa, kuweko kwa wakati mmoja Luteni Jenerali Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis mjini Baghdad makamada muhimu wa Kiirani na Kiiraqi waliokuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na wakati huo huo walikuwa kikwazo kikubwa cha Marekani kufikia malengo yake katika eneo la Asia Magharibi ilikuwa fursa ya dhahabu ambayo hawakupaswa kuicha ipite hivi hivi.

Jambo hilo limezingatiwa pia na ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa. Callamard ameandika, sababu zinazotolewa na Marekani za kuhalalisha shambulio lake la droni dhidi ya Luteni Jenerali Qassim Suleimani halina mashiko na hakuna ushahidi wowote ule wa kuweko tishio ambalo lingetokea karibuni.

Mehmet Perinçek, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Uturuki yeye anasema: Luteni Jenerali Qassim Suleimani alikuwa kikwazo kikubwa dhidi ya mipango ya kieneo ya Marekani. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana lengo la kwanza la Marekani lilikuwa ni kumuua jenerali huyo shupavu.

Agnes Callamard, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa

 

Jambo jingine ni kuwa, Marekani ilichukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa na ambayo inakinzana kikamilifu na sheria za kimataifa nayo ni kumuua kigaidi afisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa nchi nyingine pasi na kutangazwa vita baina ya nchi mbili.

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anasema kuhusiana na hili kwamba: Mwaka mmoja uliopita kulifanyika mauaji yenye malengo maalumu dhidi ya Jenerali Suleimani katika ardhi ya Iraq ambayo kimsingi lilikuwa tukio la kwanza la namna yake kufanywa na Marekani, ambapo Washington ilihalalisha mauaji hayo kwa kisingizo kwamba, hatua hiyo ilikuwa ni ya kujihami.

Kwa msimamo huu wa Agnes Callamard, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuwa kinyume na sheria za kimataifa mauaji ya Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qassim Suleimani na watu aliokuwa amefuatana nao, haibakii shaka yoyote kwamba, Trump na serikali yake ndio wakiukaji wakuu wa sheria za kimataifa na wakiwa na lengo la kusukuma mbele gurudumu la siasa zao, wako tayari kufanya chochote kile na kupuuza kabisa kanuni na sheria ya aina yoyote ile.

Tags