Jan 13, 2021 04:42 UTC
  • Waziri wa Ulinzi: Maadui wameshindwa kupigisha magoti Iran

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigedia Jenerali Amiri Hatami amesisitiza kuwa, maadui walidhani wangeipigisha magoti Iran lakini wameshindwa kabisa kutokana na Wairani kusimama kidete dhidi yao na sasa ni Rais Trump wa Markeani na waitifaki wake ndio wanaochukiwa zaidi na watu duniani na watatupwa katika dampo la taka za historia.

Brigedia Jenerali Hatami ameyasema hayo Jumanne wakati alipohutubu katika khitma ya siku ya arubaini tokea auawe shahidi mwanasayansi maarufu wa Iran Mohsen Fakhrizadeh katika Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti mjini Tehran. Amesema njia ya mashahidi Fakhrizadeh na Luteni Jenerali Qassem Soleimani itaendelezwa bila kusita na maadui wanafahamu vyema hilo.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa kijeshi amesisitiza kuwa, sayansi haiwezi kuangamizwa au kuharibiwa na hivyo maadui sasa wanatumia mbinu ya kuwaua wanasayansi.  Aidha amesema  maadui walimuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani ambaye alikuwa shujaa katika vita dhidi ya ugaidi na kuongeza kuwa Shahidi Soleimani aliwashinda magaidi wa ISIS ambao walikuwa wameteka asilimia 90 ya ardhi za Syria na Iraq. Amongeza kuwa pamoja na jitihada hizo kubwa za shahidi Soleimani, maadui walimtaja kuwa eti ni gaidi.

Ikumbukwe kuwa, magaidi wenye silaha siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba mwaka 2020 waliishambulia gari iliyokuwa imembeba Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran na kumuua shahidi mwanasayansi huyo mkubwa wa nyuklia na masuala ya ulinzi. 

Mashahidi Soleimani na Fakhrizadeh

Naye Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) aliuawa Iraq Januari 3 mwaka 2020 wakati akiwa nchini humo kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

Tags