May 08, 2021 12:25 UTC
  • Saeed Khatibzadeh
    Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, madai yasiyo na msingi yaliyotolewa hivi karibuni na serikali ya Morocco dhidi ya Iran yametolewa kwa maslahi, mipango na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo Jumamosi na kubainisha kuwa, bwabwaja za Nasser Bourita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco katika mkutano uliofanyika kwa njia ya intaneti hivi karibuni na kundi la mashinikizo la Wayahudi wa Marekani (AIPAC) yanaashiria uungaji mkono wa serikali ya Rabat kwa utawala wa kijinai wa Israel.

Amesema madai hayo yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika mkutano wa lobi ya Wazayuni si tu yametolewa kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel, lakini pia yako dhidi ya wale wote wanaounga mkono kwa dhati kadhia ya Palestina.

Khatibzadeh amesema, inasikitisha kuona, katika shabaha tu ya kuwaunga mkono maadui wa Umma wa Kiislamu, Morocco ambayo ni Rais wa Kamati ya Quds, inapotosha fikra na mazingatio kutoka kwenye kadhia kuu ya Umma wa Kiislamu, ambalo ni suala la ukombozi wa Quds tukufu na haki za Wapalestina. 

Raia wa Morocco akichoma moto bendera ya Israel

Katika mkutano huo wa AIPAC wa jana Ijumaa, siku ambayo dunia ilikuwa ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds, Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco alikariri madai yasiyo na maana eti Iran inasababisha ukosefu wa amani kaskazini na magharibi mwa Afrika.

Tarehe 10 Disemba mwaka jana 2020, Morocco ilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kuungana na nchi nyingine za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan ambazo nazo zimejidhalilisha kwa Wazayuni kwa kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel na kudharau waziwazi malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina. Siku chache baadaye, Morocco na utawala haramu za Kizayuni wa Israel zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano baina yao na kisha Marekani ikatambua rasmi mamlaka ya udhibiti wa Morocco kwa eneo la Sahara Magharibi. 

Tags