Aug 01, 2021 12:34 UTC
  • Saeed Khateebzadeh
    Saeed Khateebzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, utawala haramu wa Israel unapaswa kuacha kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran.

Akizungumzia tuhuma za Israel kwamba Iran ilihusika katika hujuma iliyolenga meli ya kubeba mafuta ya utawala huo, Saeed Khateebzadeh amesema leo Jumapili kwamba, hii si mara ya kwanza kwa utawala huo wa Kizayuni kutoa tuhuma kama hizo na kwamba ni mbinu ya muda mrefu wa utawala huo ghasibu. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema, utawala huo husababisha ukosefu wa amani, ukatili na vita popote pale unapoweka mguu na kwa msingi huo nchi zilizoufungulia mlango wa kuingia eneo hili la Magharibi mwa Asia pia zinapaswa kulaumiwa. 

Kuhusu wito uliotolewa na baadhi ya maseneta wa Marekani waliomtaka Rais wa nchi hiyo, Joe Biden azuie kuingia Marekani rais mteule wa Iran, Sayyid Ibrahim Raeisi kwa ajili ya kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa, Khateebzadeh amesema, wito huo ni wa kitoto, kipumbavu na umetolewa katika fremu ya lobi inayopiga vita Iran. Amesisitiza kuwa, Marekani inapaswa kutekeleza majukumu yake ya kuwa mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa. 

Vilevile ameashiria yanayojiri nchini Tunisia na kusema: Tehran inachunguza kwa karibuni matukio ya Tunisia na iko pamoja na taifa na serikali ya nchi hiyo katika jitihada zao za kuvuka kipindi cha sasa. Amesisitiza kuwa mazungumzo shirikishi ndiyo njia pekee ya kuvuka kipindi hiki.