Aug 02, 2021 08:12 UTC
  • Naftali Bennett
    Naftali Bennett

Kampuni ya Zodiac Maritime inayomilikiwa na bilionea wa Kizayuni, Eyal Ofer Ijumaa iliyopita ilitoa taarifa ikitangaza kuwa, meli ya Mercer Street inayomilikiwa na Israel imeshambuliwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani katika Bahari ya Oman.

Baada ya shambulizi hilo, Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett Jumapili ya jana alidai bila ya kutoa ushahidi wowote kwamba: Taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa, Iran imeshambulia meli ya Israel. 

Akijibu tuhuma za Israel na Marekani dhidi ya Iran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saeed Khateebzadeh alisema jana Jumapili kwamba, hii si mara ya kwanza kwa utawala huo wa Kizayuni kutoa tuhuma kama hizo na kwamba ni mbinu inayotumiwa kwa muda mrefu na utawala huo ghasibu. Amesema tuhuma hizo zimetolewa katika fremu ya lobi iliyoajiriwa na inayojulikana ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Marekani. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema, utawala huo husababisha ukosefu wa amani, ukatili na vita popote pale unapoweka mguu na kwa msingi huo nchi zilizoufungulia mlango wa kuingia eneo hili la Magharibi mwa Asia pia zinapaswa kulaumiwa. 

Kwa kutilia maanani harakati za kigaidi na uharibifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia, baadhi ya wachambuzi wa mambo wamezungumzia malengo ya harakati ya sasa na utawala huo. Sayyid Hadi Burhani ambaye ni mpembuzi wa masuala ya Asia Magharibi anasema: "Tunajua vyema kwamba, katika miaka kadhaa ya karibuni Israel imefanya operesheni kadhaa za uharibifu dhidi ya Iran. Kwa msingi huo kuna uwezekano kwamba, Tel Aviv ndio mhusika mkuu wa yanayojiri sasa katika Bahari ya Oman. Kuvuruga usalama wa eneo hili na kisha kuituhumu na kuitupia lawama Iran kuna maslahi kwa Israel katika kipindi na mazingira ya sasa. Baada ya Joe Biden kushika hatamu za uongozi huko Marekani kuna uwezekano wa Washington kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutatuliwa hitilafu zilizopo. Israel inapinga vikali mchakato huo na inafanya kila iwezalo kuvuruga usalama na kufanya uharibifu ili kuzuia mapatano ya aina yoyote na hatimaye kuizuia Marekani isirejee kwenye mapatano ya JCPOA."

Biden na Netanyahu

Siku chache zilizopita pia mbunge wa zamani wa Israel, Taleb Abu Arar alisema, kuna uwezekano kwamba, Israel imehusika na mashambulizi yaliyolenga meli za kubeba mafuta katika bandari ya al Fujairah, na utawala huo na washirika wake wa kikanda wanafanya njama za kuvuruga usalama na kuzusha machafuko katika eneo hili.

Hapa inatupasa kuashiria nukta mbili muhimu:

Kwanza ni kwamba, si jambo la kimantiki kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuendeleza mashambulizi dhidi ya kambi ya mapambano huko Syria, Lebanon na Yemen lakini isitarajie jibu kutoka kwa wapiganaji wa kambi hiyo. Utawala wa Kizayuni wa Israel umetumbukia katika makosa ya kimahesabu iwapo unadhani kuwa, utaendelea daima kushambulia maeneo na ngome za muqawama bila ya kujibiwa. Jibu hilo linaonesha kwamba, zama za Israel kufanya uchokozi na hujuma dhidi ya nchi yoyote bila ya jibu zimepita na kuyoyoma. Hii ni baada ya baadhi ya duru za kuaminika za kambi ya muqawama kutangaza kuwa, shambulizi lililolenga meli ya Israel kaskazini mwa Bahari ya Oman ni jibu kwa hujuma iliyofanywa hivi karibuni na utawala huo dhidi ya uwanja wa ndege wa Daba katika mkoa wa al-Qusayr nchini Syria.

Nukta ya pili ni kuhusu amani na Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Lango Bahari la Hormuz. Kuna baadhi ya pande zinazojaribu kuvuruga amani ya Ghuba ya Uajemi ili kukwamisha biashara na usafirishaji wa mafuta kupitia eneo hilo. Pande hizo ndozo zilezile zilizolitwisha eneo hili vita kadhaa katika miaka ya karibuni. 

Tunamalizia uchambuzi huu kwa kusisitiza kuwa, nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zinapaswa kutambua kuwa, kuwepo utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili hakuimarishi amani na usalama, bali kinyume chake; kwa sababu utawala huo ulianzishwa kwa ugaidi, mauaji, uvamizi na kupora ardhi ya mataifa mengine. Yumkini uvamizi wa Israel dhidi ya mataifa mengine ukaendelea kwa miaka kadhaa, lakini jambo lisilo na shaka ni kwamba, hautadumu milele. Hivyo hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu na katili hauwezi kuhalalisha uwepo wa dola hilo haramu.