Aug 03, 2021 11:28 UTC
  • Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika sherehe ya kuidhinishwa rasmi rais wa serikali ya 13; sisitizo la kulindwa thamani za Mapinduzi

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuidhinisha rasmi Sayyid Ibrahim Raisi kuwa rais wa serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sherehe maalumu iliyofanyika leo Jumanne katika Husainiya ya Imam Khomeini (MA) hapa mjini Tehran.

Katika hati ya idhinisho la urais, Ayatullah Khamenei amesema kwamba mahudhurio makubwa ya wananchi katika uchaguzi mkuu wa rais uliopita na chaguzi lao la shakhsia anayependwa na watu, mcha-Mungu na aliye na rekodi nzuri katika masuala ya uongozi nchini, wananchi wamethibitisha azma yao ya kuendelea kufuata njia angavu ya Mapinduzi yaani njia ya uadilifu, maendeleo na uhuru.

Ibrahim Raisi aliingia kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi na kushinda kwa kutumia nara ya 'Iran yenye Nguvu'. Mapambano dhidi ya ufisadi ambayo yanaendeshwa sambamba na uongozi mzuri, ni sehemu ya matakwa muhimu ya jamii ya leo. Hizo ni sifa mbili muhimu za Ibrahim Raisi ambazo amesifika kwazo kwa miaka mingi na sasa ameingia katika hatua nyingine ya utekelezaji akiwa rais wa nchi ili kudumisha mwenendo huo.

Hali inayoisubiri serikali ya Rais Raisi inaweza kuchunguzwa katika mitazamo miwili: Mtazamo wa kwanza ni kuhusu malengo ambayo yamepewa uzito katika serikali yake ya 13 kwa kutilia maanani mapungufu na matatizo ya kimaisha na kiuchumi yanayowakabili wananchi.

Rais Raisi akiwa na Rais anayeondoka madarakani Hassan Rouhani (kushoto)

Katika upande wa pili, kuna udharura na umuhimu wa kistratijia wa kutumiwa uwezo wa taifa katika kufanikisha malengo ya serikali na Mpango wa Saba wa Maendeleo. Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu katika sehemu ya hotuba yake, uwezo huo unapatikana katika sekta ya mafuta, maji, madini na majirani na muhimu kuliko yote, katika vipawa na ubunifu wa tabaka la vijana.

Kiongozi Muadhamu amesema: Bila shaka matatizo yaliyo yanaweza kutatuliwa kwa kutegemea uwezo huo kwa sharti kwamba utambuliwe vizuri na kisha juhudi kubwa za usiku na mchana zifanyika ili kunufaika nao.

Bila shaka kuna vizuizi, ugumu, usaliti na changamoto nyingi kwenye njia hiyo. Katika uwanja huo, Kiongozi Muadhamu ameashiria suala la vita vya propaganda na laini vinavyoendeshwa na maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa vita hivyo vinalenga kudhibiti fikra za waliowengi nchini. Maadui hao hutumia pesa nyingi na kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuendesha vita vya kutaka kuiangusha serikali huru na inayojitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Njama zote hizo bila shaka zinaoonyesha umuhimu wa thamani thabiti za Mapinduzi ya Kiislamu. Ni kutokana na umuhimu huo ndipo maadui wakawa wanafanya juhudi na njama zisizo na kikomo kwa lengo la kutaka kudhoofisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu kupitia mipango kama ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya serikali ya Kiislamu ya Iran.

Baadhi ya njama hizo hufanyika kwa shabaha ya kuwafanya vijana wakate tamaa na kupoteza matumaini na mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wakati huo huo mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran hayajawahi kusimamishwa hata kwa dakika moja.

Akizungumzi karibuni hivi mbele ya rais aliyeondoka madarakani leo na baraza lake la mawaziri siku ya Idul Ghadir, Kiongozi Muadhamu alizungumzia umuhimu wa serikali inayoingia madarakani kunufaika na uzoefu wa serikali za 11 na 12 na kusema: Moja ya uzoefu huo muhimu katika kipindi hiki ni kuwa watakaoingia madarakani wasiziamini kabisa nchi za Magharibi. Kwa msingi huo hampasi hata kidogo kuzitegemea nchi za Magharibi katika utekekelezaji wa mipango yenu kwa sababu mtashindwa tu bila shaka.

Raisi akikabidhiwa hati ya idhinisho la urais na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hivi sasa Sayyid Ibrahim Raisi amechukua usukani wa kuwa rais na kuiongoza serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo anakabiliwa na majukumu mazito katika uwanja huo. Katika nara zake za uchaguzi wa tarehe 18 Juni, Rais Raisi alipiga nara za kutetea mabadiliko, uadilifu, mapambano dhidi ya umasikini, ufisadi, ubaguzi, kutetea thamani za Mapinduzi, kutatua matatizo ya wananchi na kwa ufupi kubadilisha hali iliyopo nchini. Alisema: Matatizo ya hivi sasa yakiwemo ya kupanda ughali wa maisha kwa asilimia 44, kuongezeka madeni ya serikali, nakisi ya bajeti, ukosefu wa ajira na uhaba wa makazi ambayo yote yanatokana na uadui wa nje na vilevile uongozi mbaya ndani ya nchi, yote hayo yanahitajia marekebisho ya msingi na wananachi wanarajia kuona matumaini yao yaliyodhurika yakitafutiwa ufumbuzi na ponyo la kudumu.

Rais Raisi huku akisema kwamba kila mara ushauri wa Kiongozi Muadhamu unapopuuzwa nchi hukabiliwa na matatizo, amesisitiza kwamba: Tutafuatilia njia za kuondoa vikwazo lakini hatutafungamanisha maisha ya wananchi na matakwa ya wageni.