Dec 12, 2020 07:52 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon yalaani kuanzishwa uhusiano wa Israel na Morocco

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali 'mapatano' ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Morocco na utawala haramu wa Israel.

Katika taarifa, Hizbullah imezionya nchi za Kiarabu kuwa hivi karibuni zitajuta kuhusu maamuzi yao ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Juzu Alhamisi, Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. Ufalme wa Morocco umetangaza kuwa Marekani hivi karibuni itafungua ubalozi mdogo huko Sahara Magharibi.

Uamuzi huo wa Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel unafuatia uamuazi sawa na huo uliochukuliwa miezi ya karibuni na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan.

Mfalme Mohammed VI wa Morocco (kushoto), Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala wa Israel Netanyahu

Hizbullah imesema hatua hiyo ya Morocco kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni inavuruga malengo ya ukombozi wa Palestina.

Hizbullah imeongeza kuwa, kusalimu amri serikali hizo za Kiarabu kwa sera ya haadaa ya Marekani na utawala wa Kizayun mkabala wa kupata manufaa au kuondolewa vikwazo ni ndoto kwani hazitapata manufaa yaliyokusudiwa. Taarifa ya Hizbullah imesema nchi hizo za Kiarabu hivi karibuni zitajuta kwani zitagundua kuwa zimetumbukia katika mtego wa adui Muisraeli na njama zake hatari.

Harakati kaadhaa za kupigania ukombozi wa Palestina zimetoa taarifa na kulaani hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kusema huo ni usaliti wa wazi kwa Wapalestina. Aidha harakati hizo zimesema kufuatia usaliti huo, Morocco haistahiki tena kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Quds (Jerusalem) ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Tags