Jan 23, 2021 07:54 UTC
  • Baraza la Usalama lataka kufikishwa mahakamani wahusika wa miripuko ya Iraq

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa tamko kali la kulaani mashambulio ya kigaidi ya juzi Alkhamisi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad na limetaka wahusika wote mashambulizi hayo ya umwagaji wa damu wafuatiliwe kisheria na wapandishwe kizimbani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa aidha limesema katika taarifa yake hiyo kwamba inazitaka nchi zote duniani kushirikiana na serikali ya Iraq kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio husika ya umoja huo, kwa ajili ya kuwafuatilia na kuwatia mbaroni wahusika wote wa ugaidi huo.

Juzi Alkhamisi, Januari 21, 2021, kulitokea miripuko miwili mikubwa ya mabomu katika meidani ya al Tairan, katikati ya Baghdad, mji mkuu wa Iraq na kuua watu 35 wasio na hatia na kujeruhi wengine zaidi ya 110.

Vyombo vya habari vya Iraq vimetangaza kuwa waliohusika na mashamblizi hayo ya kigaidi ni raia wa Saudi Arabia. Genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na ugaidi huo. 

Magaidi wa ISIS

 

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, magaidi wa Daesh (ISIS) wasubiri majibu makali kutoka kwa wananchi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo na kusisitiza kwamba serikali yake itahakikisha mashambulizi mengine ya kigaidi hayatokei nchini humo. 

Vyombo vya habari vimemnukuu Mustafa al Kadhimi, Waziri Mkuu na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq akisema hayo jana Ijumaa katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyio na kuongeza kuwa, magaidi wametumia upenyo mdogo tu kufanya mashambulizi ya mabomu mjini Baghdad hivyo inabidi vipenyo kama hivyo viondolewe haraka.

Waziri Mkuu wa Iraq vile vile amesisitiza kuwa, sasa hivi mji wa Baghdad unafanyia kazi mkakati mkubwa wa kiusalama na wenye taathira katika kukabiliana na changamoto zijazo za kiusalama na kwamba mkakati na stratijia hiyo inasimamiwa moja kwa moja na yeye mwenyewe Waziri Mkuu wa Iraq.

Tags