May 11, 2021 07:42 UTC
  • Wapalestina wa Quds wawashukuru wenzao wa Ghaza kwa kuwapiga wanajeshi Wazayuni kwa makombora

Wapalestina wa mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wamefanya maandamano ya kutangaza kufurahishwa kwao na Wapalestina wenzao wa Ghaza kwa kuguswa na hali yao na kujibu jinai za Wazayuni huko Quds kwa kushambulia kwa makombora maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni.

Hayo yaliripotiwa jana usiku na televisheni ya al Mayadeen ambayo ilitangaza kuwa, wakazi wa eneo la Sheikh al Jarrah huko Quds wametangaza kufurahishwa sana na uungaji mkono wa wenzao wa Ukanda wa Ghaza. Ikumbukwe kuwa Wazayuni hivi sasa wanafanya jinai kubwa huko Quds na hasa katika eneo la Sheikh al Jarrah kwa lengo la kuwafukuza Wapalestina katika eneo lao hilo.

Mara baada ya kumalizika muda uliotolewa na Brigedi za al Qassam kwa Wazayuni kuacha kuwakandamiza Wapalestina wa Quds na hasa wakazi wa eneo la Sheikh al Jarrah, makundi ya wanamapambano wa Palestina yamepiga kwa makumi ya makombora, maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni.

 

Mtandao wa News Press wa habari za Palestina umeripoti kuwa, katika moja ya mashambulio hayo, gari la kijeshi la utawala wa Kizayuni limesambaratishwa na kombora la wanamuqawama wa Palestina kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Kundi la Saraya al Salaam, tawi la kijeshi la harakati ya Jihad al Islami ya Palestina limetangaza kuhusika na shambulio hilo na kusema kuwa, gari hilo la wanajeshi Wazayuni limepigwa kwa kombora aina ya Kornet.

Jana Jumatatu pia, Wazayuni waliingia ndani ya Msikiti wa al Aqsa na kukivunjia heshima tena Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Wazayuni waliwashambulia kwa mabomu Waislamu waliokuwa wanasali katika eneo hilo takatifu na kujeruhi makumi ya Waislamu hao.

Tags