May 13, 2021 02:17 UTC

Gazeti la Marekani la Washington Post limeashiria mashambulio na jinai za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) na kusema kuwa sio utawala huo tu ndio unazuia kufikiwa lengo lao tukufu la kuwa na nchi huru bali Marekani pia imekuwa na mchango mkubwa katika masaibu na matatizo ambayo yamewasibu kwa miongo kadhaa sasa.

Gazeti hilo limesema kuhusu hujuma ya karibuni ya utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji mtakatifu wa Quds kwamba jambo la kuzingatiwa kuhusu hujuma hiyo ni msimamo wa serikali ya Rais Joe Biden ambayo imezitaka pande mbili 'kujizuia na kupunguza mivutano' na wakati huo huo kulaani mashambulio ya maroketi ya Hamas na Jihadul Islami na kutetea eti haki ya Israel 'kujilinda.'

Kwa msingi huo, serikali ya Biden kama zilivyokuwa serikali nyingine za Marekani, imeamua kuunga mkono jinai za wazi wazi za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki na mashambulio makali ya ndege zake za kivita katika Ukanda wa Gaza kwa kisingizio kuwa huko ni kujitetea na kujilinda.

Kwa hakika katika miongo kadhaa iliyopita, marais wa Marekani wamekuwa wakiutetea kwa hali na mali utawala wa kigaidi wa Israel kwa kuupa mabilioni ya dola ambazo umekuwa ukizitumia kwa ajili ya kuongeza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Wapelestina na wakati hupo huo kutekeleza jinai za kutisha dhidi yao.

Unyama wa karibuni wa askari wa Israel dhidi ya Wapalestina wakiwemo watoto wadogo

Hii ni katika hali ambayo utawala wa Washington daima umekuwa ukitumia taasisi muhimu za kimataifa likiwemo Barazala Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutetea na kuunga mkono jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina. Wajuzi wa mambo wanasema kwamba ni uungaji mkono huo wa wazi wazi ndio umeufanya utawala huo umee pembe na kuzidisha jinai zake za kila siku dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Shibley Telhami, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Katika ugomvi huo Marekani katu si mtazamaji bali ni sehemu ya hujuma hiyo isiyo na uwiano, ambapo inautetea upande mmoja kwa madhara ya upande wa pili na hivyo kurefusha zaidi na zaidi njia ya kufikiwa suluhu.

Tukio muhimu katika mwenendo mzima wa uungaji mkono huo mkubwa wa serikali za Marekani kwa utawala ghasibu wa Israel lilionekana wazi katika kipindi cha utawala wa serikali ya Donald Trump. Katika kipindi cha miaka minne tu ya utawala wake, rais huyo wa zamani wa Marekani alitoa mchango na uungaji mkono mkubwa na ambao ulikuwa haujawahi kuonekana katika historia ya nchi hiyo, kwa utawala wa Tel Aviv. Serikali ya rais huyo ilitambua rasmi kukaliwa kwa mabavu na Israel milima ya Golan ya Syria, kuandaa na kutekeleza mpango wa 'Muamala wa Karne', kuunganishwa karibu asilimia 30 ya ardhi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, kutoa amri ya kuhamishiwa ubalozi wa Marekani katika mji mtakatifu wa Quds (Jarusalem) na kuutangaza mji huo kuwa mji mkuu wa Israel mnamo Disemba 2017 na vile vile kuanzisha mwenendo wa kufanywa kuwa wa kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na Israel.

Wakati huo huo Trump alikata misaada yote ya kifedha ya Marekani kwa mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Unrwa, kukata misaada kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kuitoa Marekani katika mashirika ya kimataifa kama vile Baraza la Haki za Binadamu na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO katika kulalamikia kile alichokitaja kuwa 'muelekeo ulio dhidi ya Israel', jambo ambalo lilikabiliwa na ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Hatimaye ubalozi wa Marekani ulihamishiwa Quds mnamo tarehe 14 Mei 2018, ikiwa ni katika mwaka wa sabini wa kubuniwa dola bandia la Israel. Quds Mashariki ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1967. Licha ya kuchukuliwa hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria za kimataifa lakini mji huo hautambuliki kimataifa kuwa mji mkuu wa utawala huo ghasibu. Tarehe 21 Disemba 2017 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kura 128 za ndio, 9 za hapana na 35 za kutounga mkono upande wowote, azimio la kupinga hatua ya upande mmoja ya Marekani kuutambua mji huo mtakatifu kuwa mji mkuu wa Israel na vile vile hatua yake ya kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo.

Dunia yalaani ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina wasi na hatia

Hatua hiyo ya kijuba ya Trump bila shaka iliupelekea utawala wa kibaguzi wa Irseal kuzidisha jinai na mashinikizo dhidi ya Wapalestina kwa madhumuni ya kuwabana na kuwafukuza katika eneo la Qus Mashariki kama tulivyoona ukifanya hivi karibuni katika kitongoji cha Sheikh Jarrah.

Kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Trump, utawala huo uliongeza pia mashinikizo dhidi ya waumini wa Kipalestina wanaofanya ibada katika Msikiti wa al-Aqsa ili kutoa mwanya kwa Mayahudi wenye misimamo mikali kuingia na kuuvunjia heshima msikiti huo, na hatimaye kuudhibiti kabisa. Pamoja na hayo lakini mapambano ya kishujaa na ya kupigiwa mfano ya Wapalestina katika miongo ya karibuni yamevunja kabisa njama za Wazayuni za kutaka kuyadhibiti kikamilifu maeneo matakatifu ya Waislamu na wakati huo huo kuiweka Marekani katika hali ngumu na kutojua la kufanya.

 

Tags