May 13, 2021 11:37 UTC
  • Maelfu ya Wapalestina washiriki katika Sala ya Idul Fitr kwenye Msikiti wa al Aqsa

Makumi ya maelfu ya Wapalestina wameshiriki katika Sala ya Idul Fitr leo Alkhamisi asubuhi katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu licha ya sheria kali zilizowekwa na utawala wa Kizayuni ambao siku chache zilizopita wanajeshi wa utawala huo katili waliwashambulia kwa mabomu Waislamu waliokuwa wanasali ndani ya Msikiti huo.

Idara ya Wakfu ya mji wa Quds huko Palestina imeripoti kuwa, mapema leo asubuhi, maelfu ya Wapalestina wa mji wa Quds na viunga vyake wamemiminika kwenye Msikiti wa al Aqsa na kutekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr huku wakipiga takbiri kwa sauti kubwa na kuhinikiza eneo hilo takatifu.

Idara hiyo imesema pia kwamba wanajeshi wa Israel wamewazuia mamia ya Waislamu wa Palestina kufika kwenye Msikiti wa al Aqsa na walikuwa wanaruhusu watu wazima na wenye umri mkubwa tu kuvuka vizuizi vingi vilivyowekwa na wanajeshi hao.

Hii ndiyo ilivyokuwa hali ya Kibla cha Kwanza cha Waislamu baada ya kuchomwa moto na Wazayuni

 

Taarifa ya Idara ya Wakfu ya mji wa Baytul Muqaddas huko Palestina imeongeza kuwa, licha ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kuweka vizuizi vingi vya kuwazuia Wapalestina kufika katika Msikiti wa al Aqsa na kuwazuia mamia ya Wapalestina hata wasiingie katika mji wa Quds, lakini maelfu ya Wapalestina wamefanikiwa kutekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr kwenye Msikiti huo.

Wapalestina waliofanikiwa kusali katika Msikiti wa al Aqsa wametangaza uungaji mkono wao kwa wenzao wanaodhulumiwa na kushambuliwa kikatili na Wazayuni hasa katika kitongoji cha Sheikh Jarrah na Ukanda wa Ghaza.

Ukatili wa wanajeshi wa Israel umeongezeka sana katika mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu, na utawala wa Kizayuni umefanya jinai dhidi ya Waislamu wa Palestina na Kibla cha Kwanza cha Waislamu kiasi kwamba hata watu wasio Waislamu wanaendelea kulaani jinai hizo.

Tags