May 16, 2021 06:43 UTC
  • UN yashindwa tena kulaani jinai za Israel huko Gaza, yatosheka kwa kueleza masikitiko

Sambamba na mashambulizi makali na ya kinyama yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya raia wa Ukanda wa Gaza, na mauaji ya raia katika eneo hilo, Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena umeshindwa kuchukua hatua ya maana ya kusimamisha mashambulizi hayo au hata kulaani kwa maneno hujuma na ukatili huo wa Israel.

Kikao cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana kujadili hali ya Palestina kilitosheka tu kwa kueleza masikitiko yake kuhusiana na mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres imeeleza wasiwasi wa kiongozi huyo kutokana na kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kutangaza kuwa: Mashambulizi ya aina yoyote yanayolenga raia na vyombo vya habari yanakiuka sheria za kimataifa na yanapaswa kuepukwa. 

Guterres ameashiria mashambulizi ya jeshi la Israel yanayolenga makazi ya raia katika Ukanda wa Gaza na kusema: Umoja wa Mataifa unasikitishwa na idadi kubwa ya raia wanaouawa katika hujuma za Israel wakiwemo watu 10 wa familia moja waliouawa katika hujuma ya Israel dhidi ya kambi ya wakimbizi ya  Shat'i. 

Makumi ya watoto na wanawake wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel, Gaza

Mapema jana jeshi katili la utawala ghasibu wa Israel lilishambulia vikali maeneo kadhaa ya Gaza ikiwemo Benki ya Taifa ya Kiislamu, Hospitali ya al Shifaa na ofisi ya Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas. Jeshi la Israel pia limeshambulia na kubomoa kabisa jengo kubwa la mashirika kadhaa ya habari ya kimataifa ikiwemo televisheni ya al Jazeera ya Qatar na shirika la habari la Associated Press mjini Gaza.  

Tags