May 21, 2021 12:14 UTC
  • Palestina kuushitaki utawala wa Kizayuni katika mahakama ya ICC

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani wa Palestina amesema kuwa, mamlaka hiyo itaishitaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kwa jinai zake za kuua watoto wadogo na wanawake wa Wapalestina wasio na hatia.

Shirika rasmi la habari la Palestina WAFA limemnukuu Mohammad Shtayyeh akisema hayo leo Ijumaa na huku akishukuru juhudi za kimataifa za kukomesha uvamizi na ukatili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ghaza, amelalamikia vikali kushindwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa angalau tamko la kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni.

Vile vile amesema, jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 11 vilivyomalizika jana usiku ikiwa ni pamoja na kuua kikatili wanawake na watoto wadogo wa Kipalestina zitafunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. 

Watoto wadogo, wahanga wakuu wa jinai za Israel Palestina

Waziri Mkuu huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina vile vile amesema, mahakama ya ICC tayari imeshaanza kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vitatu vya huko nyuma dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza. 

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kufurahishwa kwake na kuanza kutekelezwa usimamishaji vita huko Ghaza.

Vita vya siku 11 vilivyomalizika jana usiku, vilianza baada ya utawala wa Kizayuni kuvamia na kuharibu nyumba za wakazi wa eneo la Sheikh Jarrah huko Baitulmuqaddas Mashariki na vile vile kukivunjia heshima Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa.

Katika taarifa yake, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kushirikiana kikamilifu na umoja huo kwa ajili ya kuwasaidia waathiriwa wa vita huko Palestina.

Tags