May 23, 2021 02:50 UTC
  • Hasara za kiuchumi zilizosababishwa na vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza

Vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vimemalizika baada ya kusababisha hasara kubwa za kiuchumi hususan kwa utawala wa Kizayuni wa Israel wenyewe.

Hasara za kiuchumi za vita hivyo tunaweza kuzigawa katika sehemu mbili, hasara za vita kwa eneo la Gaza na zile zilizoupata utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kipindi chote cha siku 12, Israel ilifanya mashambulizi elfu mbili ya anga dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Viongozi wa Gaza wanasema zaidi ya nyumba 1,447 za raia zimeharibiwa kikamilifu katika mashambulizi hayo. Vilevile nyumba nyingine elfu 13 zimepatwa na madhara katika mashambulizi hayo ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Maafisa wa Gaza pia wanasema, jeshi la Israel lilikuwa likilenga kwa makusudi miundombinu na taasisi zote za huduma za kiraia na vituo vya kiuchumi na kwamba mashambulizi ya utawala huo yamesababisha uharibifu mkubwa katika mtandao wa kusambaza maji na barabara za mawasiliano. Raid Jarrar ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Viwanda katika Wizara ya Uchumi ya Gaza anasema: "Zaidi ya viwanda 50 vimeharibiwa katika mashambulizi ya siku 12 ya Israel. Aidha Kitengo cha Upashaji habari cha serikali ya Palestina katika eneo la Gaza kimetangaza kuwa, mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yamesababisha hasara ya dola milioni 322."

Jengo la mashirika ya habari la al Jalaa, Gaza

Takwimu zinaonesha kuwa, hasara za Israel katika vita hivyo ni zaidi ya hasara zilizosababishwa na mashambulizi ya utawala huo huko Gaza. Muhammad Abu Rizq ameandika katika mtandao wa Khalij Online kwamba: "Hasara za kibinadamu si hasara pekee zilizoipata Israel katika vita vya siku 12, bali kutokana na majibu makali ya wanamapambano wa Palestina, utawala huo wa Kizayuni pia kila siku ulikuwa ukipata hasara ya mamilioni ya dola kutokana na kufungwa viwanja vya ndege, kuporomoka masoko ya hisa na mabenki kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa na inaripotiwa kuwa, thamani ya sarafu ya Israel imepungua kwa asilimia 14 ikilinganishwa na dola ya Marekani."

Mbali na hayo Israel imepata hasara kubwa kutokana na kutumia mfumo wa ulinzi wa Iron Dome. Mtaalamu wa masuala ya uchumu Ahmad Musbih anasema: "Hasara za kiuchumi za utawala wa Kizayuni kutokana na vita dhidi ya Gaza ni kubwa sana. Israel imetumia gharama kubwa kutengeneza makombora na mfumo wa ulinzi wa Iron Dome ili kuzuia madhara na hasara kama hizo, lakini haikufanikiwa."

Afisa mmoja wa Wizara ya Fedha ya Israel amesema baada ya kutangazwa usitishaji vita huko Gaza kwamba, hasara zilizosababishwa na vita hivyo ikilinganishwa na hasara za vita vya siku 51 vya mwaka 2014 ambayo ilifikia asilimia 0.3 ya uzalishaji ghafi wa ndani, imefikia karibu asilimia 0.5 ya uzalishaji ghafi wa ndani wa Israel ambao ni sawa na dola bilioni 2. Hii ni licha ya kuwa, muda wa vita vya mwaka 2014 ni zaidi ya mara nne ya muda ya vita vya sasa vya Gaza. 

Hizi ni hasara zlizokadiriwa na Israeli yenyewe. Vilevile inatupasa kuelewa kwamba, vita hivi pia vina hasara za muda mrefu kwa utawala huo wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na kuondoka wawekezaji wa kigeni katika masoko ya Israel kutokana na ukosefu wa amani. Gazeti la masuala ya uchumi la TheMarker la Israel limeripoti kuwa, asilimia 17 ya viwanda vya maeneo ya kusini mwa Israel na Tel Aviv vimefungwa. Gazeti hilo limesisitiza kuwa, kuna hasara nyingine nyingi ambazo zitadhihiri baada ya kumalizika vita na kubainika vyema hasara za kiuchumi za Israel kama kufungwa safari za ndege katika viwanja vya Ben Gurion na Ramon na vilevile kufutwa safari za kitalii.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Nukta nyingine ya kuashiriwa hapa ni kwamba, vita vya sasa vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza vitakuwa na taathira nyingi mbaya kwa ustawi wa kiuchumi wa utawala huo. Israel ilikadiria kwamba, uchumi wa utawala huo utastawi kwa asilimia 6.3 mwaka huu wa 2021, lakini sasa jambo hilo litakuwa muhali kutokana na athari mbaya na za muda mrefu za vita vya siku 12 huko katika ukanda wa Gaza.   

Tags