May 24, 2021 10:06 UTC
  • Utambulisho wa kigaidi wa Israel wabainika zaidi baada ya tishio la kuwaua makamanda wa muqawama

Benny Gantz waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa tishio la wazi la kutaka kuwaua kigaidi makamanda wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.

Mbinu ya mauaji ya kigaidi imekuwa ikitumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel tokea mwanzo wa kuasisiwa kwake. Miezi kadhaa baada ya kuundwa utawala wa Kizayuni wa Israel mbinu ya kuwaua kinyama mahasimu ilianza kutumiwa na utawala huo. Mwaka wa 1948 mjini Quds (Jerusalem) genge la  Wazayuni linalojulikana kama Lehi lilimuua mwanadiplomasia mwandamizi wa Sweden Folke Bernadotte ambaye alikuwa mpatanishi wa Umoja wa Mataifa baina ya Waarabu na Israel.  Bernadotte alikuwa amewasilisha mpango ambao ulikuwa na mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kusitishwa hatua ya Mayahudi kuhamia katika ardhi za Palestina na kubakia mji wa Quds chini ya usimamizi kamili wa Waarabu.

Katika muongo wa 1950 utawala wa Kizayuni ulitekeleza mauaji kama sera yake ya kimsingi bila kujali madhara ya kisiasa na kisheria ya ukatili huo.

Askari wa jeshi la kigaidi wa Israel akiwa amemkamata mtoto Mpalestina

Ronen Bergman mwandishi habari wa masuala ya kiusalama na kijeshi wa Israel katika kitabu alichokipa anwani ya 'Rise and Kill First' na kukichapisha mwaka 2018 anasema: "Katika kipindi cha uhai wake wa miaka 80, utawala wa Kizayuni wa Israel umetekeleza karibu oparesheni 2700 za mauaji." Noam Chomsky mwanafikra wa Kimarekani hivi karibuni alisema stratijia ya mauaji ya kisiasa ni msingi wa utawala wa Israel.

Hivi sasa pia Benny Gantz, waziri wa vita wa  utawala wa Kizayuni ametishia kuwa atamuua Yahya Sinwar, kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Ghaza na Mohammad Dheif kamanda wa Brigedi za Qassam, Tawi la Kijeshi la Hamas. Titishio hilo la wazi la Gantz linaashiria nukta kadhaa muhimu.

Kwanza ni kuwa wakati utawala wa Kizayuni wa Israel unaposhindwa katika vita huanza kutekeleza mauaji ya kigaidi ambayo huwa mbinu khabithi zaidi.

Hivi sasa baada ya utawala huo kushindwa katika vita vya siku 12 umeelekeza nguvu zake zote katika kuwaua makamanda wa ngazi za juu wa Hamas ili kwa dhana yake potovu, harakati ya muqawama ipate pigo kwa mtazamo wa nguvu kazi na uzoefu na hivyo itumbukie katika matatizo. Hii ni katika hali ambayo Hamas na makundi mengine ya muqawama yameweza kuthibitisha mara kadhaa kuwa, kila mara makamanda wa muqawama wanapouawa shahidi, azma ya kupambana na Israel na kuupa pigo utawala huo huimarika maradufu.

Yahya Sinwar

Nguvu za makombora ambazo zimeonyeshwa na harakati za ukombozi wa Palestina au muqawama katika vita vya siku 12 ni natija ya kuuawa shahidi makamanda wa muqawama.

Nukta ya pili ni kuwa waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametangaza wazi na bayana kuwa atawaua makamanda wa ngazi za juu wa Hamas. Kwa maneno mengine ni kuwa, Israel  inapuuza na haitilii maanani sheria na kanuni za kimataifa kwa sababu inafahamu kuwa jamii ya kimataifa haitaichukulia hatua zozote.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki Ijumaa iliyopita baada ya kuanza kutekelezwa usitishwaji vita baina ya Israel na makundi ya mapambano ya Palestina alisema Israel ni utawala ghasibu na wa kigiadi na sasa umefika wakati wa dunia kutofumbia macho ukweli huu.

Na nukta ya tatu ni kuwa tishio la mauaji ya kigaidi haliwaogopeshi makamanda wa muqawama bali wako tayari kukumbatia kuuawa shahid kwani kuwa tayari kuuawa shahidi ni katika thamani za dini tukufu ya Kiislamu. Kwa msingio huo katika hali ambayo Gantz anatoa vitisho dhidi ya viongozi wa Hamas katika Ukanda wa Ghaza, siku ya Jumamosi Sinwar alionekana katika mitaa ya Ghaza ambapo katika hatua ya kwanza alifika katika nyumba ya Shahidi Bassim Isa,mmoja kati ya makamanda wa Brigedi za Qassam.

 

Tags