Jun 07, 2021 02:29 UTC
  • Hamas yaonya kuhusu hujuma yoyote ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika Ukanda wa Ghaza ametoa tamko baada ya kubainika kuwa Wazayuni wanapanga kufanya shambulio jingine dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Yahya Sinwar kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Ghaza ameonya kuwa, iwapo Wazayuni watauhujumu tena msikiti wa al Aqsa basi harakati  za muqawama na mapambano zitauharibu mji wa Tel Aviv.

Akizungumza na Shirika la Habari la Palestina la SAFA ameashiria wito wa magenge yenyemisimamo ya kufurutu ada ya Israel kuhusu kile ambacho magenge hayo yamekitaja kuwa ni 'maandamano ya bendera' katika mji wa Quds siku ya Alkhamisi na kusema: "Iwapo Wazayuni watarejea tena na kuuhujumu Msikiti wa al Aqsa, sisi pia tutarejea na hilo kwetu halina shaka."

Yahya Sinwar

Magenge ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada yametoa mwito kwa Wazayuni kushiriki katika maandamano ya kichochezi siku ya Alkhamisi katika Msikiti wa Al Aqsa ambapo gazeti la Kizayuni ya Yedioth Ahronoth limesema Wazayuni hao wanasubiri idhini ya polisi ya Israel.

Msemaji wa Hamas Mohammad Hamada naye pia ametoa taarifa  kuhusu njama hiyo ya Wazayuni ya kuuvamia msikiti wa al Aqsa ambapo ameuonya utawala wa Kizayuni usijaribu kujipapatua kwenye makucha ya migogoro mikubwa ya ndani ya Israel kupitia kuzusha ghasia mjini Quds.

Aidha amewataka Wapalestina huko Baytul Muqaddas kujitokeza kwa wingi na chukua hatua imara za kuulinda Msikiti wa al Aqsa siku hiyo ya Alkhamisi.

Tags