Jul 08, 2021 04:19 UTC
  • Zaidi ya wasomi, wanafikra 600 wa kimataifa wataka kuvunjwa utawala wa kibaguzi katika Palestina ya kihistoria

Idadi kubwa ya wasomi, wasanii na wanafikra kutoka nchi nyingi duniani wametoa wito wa kuvunjwa mfumo wa ubaguzi wa rangi ulioanzishwa katika ardhi za Palestina ya kihistoria, na kuanzishwa mfumo wa utawala wa kidemokrasia ambao utatoa haki na majukumu sawa kwa wakazi wote wa nchi hiyo bila ubaguzi wowote kwa misingi ya rangi, mbari, dini au jinsia.

Mtandao wa Mediapart wa Ufaransa umeripoti kuwa, zaidi ya wasomi, wasanii na wanafikra 600 kutoka nchi zaidi ya 45 wametia saini tamko la kutaka kuvunjiliwa mbali utawala wa ubaguzi wa rangi katika ardhi ya kihistoria ya Palestina (Israel).

Miongoni mwa waliotia saini tamko hilo wamo watu mashuhuri na washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kama vile Muargentina Adolfo Pérez Esquivel, anayejulikana kwa kutetea haki za kibinadamu, Mu-Ireland, Mairead Maguire, maarufu kwa kutetea amani, mawakili Monique Chemilier-Gendreau ambaye ni profesa wa sheria za umma, na Richard Falk, mwandishi na mwanaharakati wa Marekani katika masuala ya kimataifa.

Tamko hilo ambalo limetolewa kwa anwani ya "Azimio la Kutokomeza na Kuadhibu Wahalifu wa Ubaguzi wa Rangi katika Palestina ya Kihistoria", limetoa mifano kadhaa ya uhalifu wa Israel, yakiwemo maafa ya Nakba ya tangu miaka 73 iliyopita ambayo ni pamoja na kuhamishwa Wapalestina kwa nguvu kutoka kwenye makazi yao, kuangamizwa kizazi chao, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Miongoni mwa uhalifu huo ni kuanzishwa utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wa Palestina na kuwatambua Wayahudi kuwa ndiyo jamii bora zaidi kuliko watu wengine. 

Tamko hilo pia limetaja mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, mauaji ya idadi kubwa ya raia wasio na hatia na mzingiro wa kikatili wa miaka 14 sasa dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

Tamko hilo limesisitiza kuwa, madola ya Magharibi yameuwezesha na kuunga mkono utawala huo wa kibaguzi wa Israel ulioasisiwa kwa msingi wa maangamizi ya kizazi na ubaguzi wa rangi kwa zaidi ya miongo 7, na kwamba nchi hizo za Magharibi bado zinauhami na kuunga mkono utawala huo kidiplomasia, kiuchumi na hata kijeshi.   

Vilevile wamezihimiza nchi zao kukomesha mara moja uhusiano wao na utawala wa kibaguzi wa Israel na zijiunge na wito wa kuvunjwa utawala huo. 

Wasomi, wanafikra na wasanii hao pia wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya viongozi wa kisiasa wa Israeli na wafanyikazi wa masuala ya usalama wanaotuhumiwa kafanya uhalifu wa ubaguzi wa rangi.

Tags