Jul 09, 2021 03:40 UTC
  • OCHA yatoa indhari: Idhini ya UN ya ufikishaji misaada ikisitishwa maisha ya Wasyria yatakuwa hatarini

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, imetahadharisha kuwa ifikapo tarehe 10 mwezi huu wa Julai, endapo muda wa idhini ya Baraza la Usalama la UN ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Syria hautarefushwa, mateso ya raia hao yataongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 10 ya mgogoro wa nchi hiyo.

Mamilioni ya Wasyria wanategemea misaada ya UN inayotolewa chini ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pande zote za mpaka kuruhusu misaada hiyo kuvushwa. 

Mark Cutts, Naibu Mratibu wa masuala ya  Kibinadamu wa Kikanda kwa upande wa Mgogoro wa Syria katika Umoja wa Mataifa anasema, "kuna watu milioni tatu na laki nne upande wa pili wa mpaka, ambao tunawapa chakula, dawa, mahema, blanketi, na vifaa vingine vya msaada vinavyohitajika haraka. Kushindwa kuendeleza azimio la Baraza la Usalama kwa shughuli hii ya kuvuka mpaka itawanyima mamilioni ya watu ambao wamenaswa katika eneo la vita msaada ambao wanauhitaji kwa maisha yao." 

Muongo mmoja wa vita na kuanguka kwa uchumi kumewaacha zaidi ya watu milioni 13 nchini Syria wakihitaji msaada wa kibinadamu. Baadhi ya mahitaji muhimu zaidi yako kaskazini magharibi mwa nchi ambapo watu milioni 4 na laki mbili hasa wanawake na watoto, wamenaswa katika eneo la vita karibu na mpaka wa Syria na Uturuki. 

Inafaa kuashiria kuwa operesheni ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Syria hivi sasa ni kubwa zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ulimwenguni.../

 

Tags