Jul 19, 2021 01:22 UTC
  • Hamas  yatoa wito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi katika Msikiti wa Al Aqsa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetoa wito kwa umma wa Palestina kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya Itikafu ndani ya Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) kwa lengo la kulinda eneo hilo takatifu ambalo linakabiliwa na hujuma ya walowezi wa Kizayuni wanaopata himya ya utawala ghasibu wa Israel.

Kwa mujibu wa tovuti ya Felestin Al Youm, Mohammad Hamada, Msemaji wa Hamas mjini Quds  ametangaza Jumapili kuwa, hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Al Aqsa chini ya himaya ya askari wa utawala wa Kizayuni haziashirii satwa yao katika msikiti huo bali ni ishara ya kushindwa maghasibu hasa baada ya makabiliano ya hivi karibuni.

Hamada ametoa wito kwa Wapalestina wajitokeze kwa wingi kuelekea Quds Tukufu hasa katika Msikiti wa Al Aqsa kwa lengo la kushiriki katika Itikafu Msikitini hapo kabla ya Siku Kuu ya Idul Adha na pia kuulinda msikiti huo mkabala wa Wazayuni maghasibu.

Kwa upande wake, Tariq Salmi, msemaji wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ameashiria hujuma ya kinyama ya askari wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa Jumapili asubuhi na kusema, 'hivi sasa katika msikiti wa Al Aqsa tunashuhudia ugaidi na uvamizi ambao unaumiza nyoyo za Waislamu wote duniani.

Sheikh Ikrima Sabri

Aidha amelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema wakati ambao adui Mzayuni anahujumu moja kati ya maeneo matakatifu zaidi kwa Waislamu, baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wanaanzisha uhusinao na utawala huo.

Kwa upande wake, Sheikh Ikrima Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al Aqsa amekosoa vikali kimya cha mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kuhusiana na matukio ya hujuma na uvamizi dhidi ya msikiti wa al-Aqsa.

Sheikh Sabri amesema kuwa, kile kinachojiri katika msikiti wa al-Aqsa, kuanzia hujuma, uvamizi na kuuvunjia heshima msikiti huo ni jinai kubwa.

 

Tags