Jul 23, 2021 02:33 UTC
  • Israel yawatia mbaroni wanachama zaidi ya 120 wa Hamas katika Ukingo wa Magharibi

Televisheni moja ya Kizayuni inayotangaza kwa lugha ya Kiibrania imetangaza kuwa Israel miezi miwili iliyopita iliwatia mbaroni wanachama zaidi ya 122 wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan.

Televisheni ya Risht Kun imedai kuwa, utawala wa Kizayuni umewatia mbaroni wanachama hao wa Hamas ili kuzuia ujenzi wa miundombinu katika Ukingo wa Magharibi. Israel imefanya kamatakamata hiyo katika miezi miwili iliyopita hususan baada ya vita vya karibuni katika Ukanda wa Ghaza mashuhuri kama "Saiful Quds."  

Vita vya siku 12 katika Ukanda wa Ghaza 

Televisheni hiyo ya Kizayuni imeongeza kudai kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 hadi sasa Israel imezuia karibu shekel milioni tatu, sarafu ya utawala wa Kizayuni ambayo ni sawa na takribani zaidi ya dola laki tisa, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli za Hamas huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan.

Taasisi za kiraia za Palestina hivi karibuni zilieleza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wamewakamata Wapalestina wasiopungua 5,426 wakiwemo wanawake na watoto. 

Tags