Jul 23, 2021 07:52 UTC
  • Mkuu wa zamani wa haki za binadamu wa UN kuongoza uchunguzi wa jinai za Israel

Baraza la Haki za Binadamu limemteua Navi Pillay, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuongoza kamati ya kimataifa ya watu watatu ya kuchunguza jinai za kivita za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa yake ya jana Alkhamisi, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limesema Pillay, jaji wa zamani wa Afrika Kusini ambaye alikuwa Kamisha Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN baina ya mwaka 2008 na 2014, ataongoza timu hiyo ya uchunguzi, iliyotwikwa jukumu la kuchunguza ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu na kukanyagwa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu ikiwemo Quds mashariki.

Kamati hiyo itachunguza chimbuko na sababu za kujitokeza mara kwa mara hali ya taharuki, ukosefu wa uthabiti, kupanuka mgogoro ukiwemo ubaguzi wa kimfumo na ukandamizaji na manyanyaso kwa misingi ya utaifa, ukabila na udini katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Pillay ataungana na Miloon Kothari wa India, Ripota Maalumu wa kwanza wa UN kuhusu uhaba wa makazi na Chris Sidoti, mtaalamu wa sheria za haki za binadamu raia wa Australia, na wanatazamiwa kuwasilisha ripoti yao ya awali mnamo Juni mwaka ujao 2022.

Shambulio la Israel dhidi ya ofisi za vyombo vya habari vya kimataifa Gaza

Rasimu ya azimio la kuundwa jopo hilo kwa azma ya kuwatambua na kuwawajibisha wahusika wa jinai za kivita huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliwasilishwa na Pakistan kwa niaba ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC); na ikapasishwa kwa kura 24 kati ya 47 za nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu. 

Itakumbukwa kuwa, Wapalestina zaidi ya 260 wakiwemo watoto wadogo 66 waliuawa shahidi katika vita vya siku 12 katika Ukanda wa Gaza vilivyoanza Mei 10 mwaka huu. Hata hivyo makundi ya muqawama yalijibu chokochoko hizo za Israel kwa kuvurumisha makombora na maroketi 4000 kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel kama Tel Aviv, Haifa na Nazareth.

Tags