Jul 30, 2021 12:37 UTC
  • Meli ya Israel yashambuliwa katika pwani ya Oman

Jeshi la Uingereza limetangaza habari ya kushambuliwa meli ya mizigo ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika pwani ya Oman.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema meli hiyo ya kibiashara inayomilikiwa na utawala haramu wa Israel ilishambuliwa usiku wa kuamkia leo karibu na kisiwa cha Masira, katika Bahari ya Kiarabu.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na wizara hiyo imeongeza kuwa, hujuma hiyo ya jana usiku ilitokea umbali wa kilomita 280 kaskazini mashariki mwa bandari ya Oman ya Duqm, yapata kilomita 300 kusini mashariki mwa mji mkuu, Muscat.

Bila kutoa maelezo ya kina, Shirika la Kusimamia Operesheni za Meli za Kibiashara la Uingereza limesema shambulio hilo si la kiharamia, lakini uchunguzi wa kubaini chanzo na wahusika wa shambulio hilo umeanza.

Ramani inayoonesha Bahari ya Oman

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, shambulio dhidi ya meli hiyo inayosimamiwa na kampuni ya mabaharia ya Zodiac Maritime ya bwanyenye wa Kizayuni Eyal Ofer ni la kiharamia.

Taarifa ya kampuni hiyo yenye makao yake mjini London imesema, meli hiyo ilishambuliwa kaskazini mwa Bahari ya Hindi, ikitokea katika mji wa bandari wa Dar es Salaam nchini Tanzania, ikielekea katika bandari ya Imarati ya Fujaira.

Katika miezi ya hivi karibuni, meli za utawala haramu wa Israel zimekuwa zikishambuliwa baharini katika maeneo mbali mbali ya dunia.

Tags