Jul 31, 2021 02:39 UTC
  • Safari ya Qalibaf mjini Damascus; ukurasa mpya wa uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Syria

Katika safari yake ya karibuni nchini Syria, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameonana na kuzungumza na rais, waziri mkuu, waziri wa mambo ya nje na wafanyabiashara wa nchi hiyo.

Katika mazungumzo yake na Rais Bashar al-Asad wa Syria hapo siku ya Jumatano, Qalibaf alisema, mashinikizo ya juu zaidi ya nchi za Magharibi na hasa Marekani dhidi ya mataifa mawili ya Iran na Syria yameshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na kwamba miaka minne ijayo itayaandalia mataifa haya fursa nzuri ya kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi.

Kwa upande wake Rais Asad amesema katika mazungumzo hayo kwamba Iran na Syria ni washirika wakubwa na kuwa kamati za pande mbili zinapasa kuanzishwa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kicuhumi wa pande mbili. Safari ya Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu nchini Syria na ambayo imefanyika baada ya nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu ambapo Rais Asad aliibuka mshindi, ina umuhimu mkubwa. Chaguzi kuu zimefanyika kwa karibu wakati mmoja katika nchi mbili na bila shaka mabunge ya nchi hizi yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi wa pande mbili.

Qalibaf katika mazungumzo na Rais Bashar al-Asad wa Syria

Kunyanyuliwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi jirani na rafiki za eneo ni kipaumbele cha duru ya 11 ya Majlisi ya Kiislamu na pia serikali mpya ya Iran na bila shaka mtazamo huo wa pamoja unachangia pakubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na nchi za Asia Magharibi na hasa Syria.

Baada ya mapambano ya muda mrefu na makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na nchi za Magharibi na washirika wao wa kieneo, Syria hivi sasa inapitia kipindi cha utulivu na uthabiti wa kisiasa na kiusalama wa kuridhisha, ambapo serikali ya nchi hiyo imetoa kipaumbele kwa ukarabati wa miundomsingi iliyoharibiwa katika kipindi cha vita. Ni wazi kuwa hiyo ni fursa nzuri kwa mashirika ya Iran kuweza kushiriki katika ukarabati huo.

Katika uwanja huo, Ali Nikzad, Naibu Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mahojiano na shirika la habari la Irna kuhusu umuhimu wa safari ya Qalibaf nchini Syria kwamba, kwa kutilia maanani hali ya Syria, Iran inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuwekeza katika nyanja za uchumi, huduma za kiufundi na kiuhandisi, ukarabati wa miji, ujenzi wa nyumba na vile vile sekta za kilimo, umeme, maji, madini na nishati nchini humo.

Syria ina fursa nyingi kwa manufaa ya mashirika ya Kiirani katika sekta mbali mbali za uchumi, biashara, viwanda na masuala ya kiufundi na kiuhandisi. Bila shaka mashirika ya Iran yana uwezo mkubwa na wa kupigiwa mfano katika nyanja hizo zote, na yanaweza kuwekeza Syria na hivyo kuwa na mchango muhimu katika ukarabati wa nchi hiyo na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Syria.

Qalibaf katika mazungumzo na spika mwenzake wa Syria Hammoud Sabbagh

Ushirikiano wa kisiasa na kistratijia wa Iran na Syria unaweza kuwa msingi mzuri kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi wa nchi mbili na fursa mpya iliyojitokeza kati ya nchi hizo inaweza kufungua ukurasa mpya wa mashirikiano ya kiuchumi ya pande mbili.

Katika kuanzishwa mapatano mapya shirikishi, Iran na Syria zinaweza kuwa mfano mzuri wa ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili na bila shaka kadiri ushirikiano huo utakavyoimarishwa ndivyo utakavyoziwezesha nchi hizo kukabiliana na hatimaye kushinda mashinikizo ya juu kabisa ya maadui wao.

Tags