Aug 02, 2021 03:57 UTC
  • Rais wa Afghanistan: Taliban wamezidi kuwa madhalimu na kuzidi kuwa hawana Uislamu kuliko walivyokuwa kabla

Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan amelikosoa vikali kundi la Taliban kutokana na linavyoshupalia vita na akasema: kundi hili limekuwa dhalimu zaidi na la kimamluki zaidi kuliko lilivyokuwa huko nyuma.

Ashraf Ghani ameyasema katika kikao cha baraza la mawaziri na akaeleza kwamba, kwa kuiandama na kuilenga serikali na wananchi, kundi la Taliban limeonyesha kuwa ikilinganishwa na hapo kabla, limekuwa la kidhalimu zaidi, limezidi kuwa halina Uislamu na halina irada wala utashi wowote wa kufikia suluhu na kurejesha amani katika nchi hiyo.

Rais wa Afghanistan ameongezea kusema: "Taliban halina imani yoyote juu ya amani na mazungumzo, isipokuwa kama sisi tutabadilisha mlingano katika medani ya vita."

Aidha amesema: Watu katika baadhi ya maeneo ya nchi hawaridhishwi na serikali, lakini serikali inataka katiba itekelezwe sawasawa ili wananchi waridhike.

Wanamgambo wa kundi la Taliban

Ashraf Ghani amelituhumu pia kundi la Taliban kwa kusema uongo na akasema, bila kubadilika hali ya usalama ya nchi, kundi hilo halitakubali kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu na amani.

Matamshi hayo ya Ashraf Ghani yametolewa katika hali ambayo, hivi sasa vita vimepamba moto katika akthari ya majimbo ya Afghanistan; na kila siku idadi ya raia na wanajeshi wanaouawa katika vita hivyo inazidi kuongezeka, huku hali mbaya ya kukosekana usalama ikizidi kutawala katika miji mbalimbali mikubwa ya nchi hiyo.../

Tags