Dec 12, 2020 07:21 UTC
  • Iran: Marekani inawashawishi wengine watoe muhanga kadhia ya Palestina

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Marekani inazishawishi nchi zingine kutoa muhanga kadhia ya Palestina na kuwapa mkono wezi kwa njia mbali mbali.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter Ijumaa usiku, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: "Marekani inajaribu kuwashawishi wengine watoe muhanga kadhia ya Palestina na kuwapa mkono wezi." Taarifa hiyo imesema Marekani imetumia vishawishi kama vile kuziondoa nchi katika orodha bandia nyeusi, mauzo ya ndege za kivita za F-35s au kutambua rasmi ukaliwaji mabavu na kutoa muhanga malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema mbinu hiyo ambayo Marekani inaitumia si ya amani na wala si udiplomasia bali ni utumiaji mabavu na utoaji rushwa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mbinu kama hiyo haitadumu kwa muda mrefu.

Ikulu ya White House ya Rais wa Marekani imesema mauzo ya silaha ni mbinu inayotumiwa kuunga mkono sera za kigeni za Marekani na ni kwa msingi huo ndio Umoja wa Falme za Kiarabu umeuziwa idadi kubwa ya silaha hivi karibuni. Baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain kutangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, Marekani imeafiki kuiuzia UAE ndege 50 za kivita aina ya F-35 na mabomu zaidi ya 14,000.

Mfalme wa Morocco Mohammed VI

Aidha Marekani imedai kuwa itaiondoa Sudan katika orodha yake ya eti nchi zinazounga mkono ugaidi, baada ya wakuu wa Khartoum kutangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel. 

Alhamisi pia Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. 

Hatua hizo za nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel zinaendelea kukosolewa na kulaaniwa vikali na viongozi wa Palestina pamoja na wapenda haki kote duniani wakisema kuwa ni usaliti wa wazi kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.

Tags