Dec 12, 2020 11:36 UTC
  • Muamala wa Trump kwa ajili ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni

Rais Donald Trump wa Marekani juzi Alhamisi alituma ujumbe katika ukurasa wake wa twitter na kueleza kuwa Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Trump amesisitiza kuwa amesaini taarifa ya kutambua rasmi mamlaka ya Morocco huko Sahara Magharibi mkabala na kuanzishwa uhusiano baina ya nchi hiyo na Israel. Sambamba na hilo, Morocco pia imethibitisha kuwa  uhusiano huo wa kawaida kati yake na utawala wa Kizayuni utaanza siku chache zijazo. Mfalme wa Morocco ametangaza kuwa Marekani imetambua rasmi mamlaka ya Morocco juu ya eneo la Sahara Magharibi na kusema kuwa hatua hiyo imebadili tukio la kihistoria. Wakati huo huo ofisi ya ufalme wa Morocco imetangaza kuwa Marekani hivi karibuni itafungua ubalozi wake mdogo huko Sahara Magharibi katika fremu ya mapatano hayo ya kuanzisha uhusiano wa kidplomasia kati ya nchi hiyo na Israel.  

Mfalme Mohamme wa Sita wa Morocco 

Kitendo hicho cha Morocco cha kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ambacho kwa yakini ni sawa na kusaliti malenngo ya Palestina kimekabiliwa na radiamali hasi katika Ulimwengu wa Kiislamu na hata ndani ya Morocco kwenyewe. 

Ili kukabiliana na hatua hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, Ahmad Vihaman Mkuu wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Morocco amesema: Taifa la Morocco linatambua malengo ya wananchi wa Palestina kuwa ni kadhia yao na kuamini kuwa kuhuisha uhusiano na utawala wa Isarel ni kuisaliti Palestina. 

Katika kipindi cha utawala wa Donald Trump Marekani imetekeleza hatua ambazo hazijawashi kushuhudiwa huko nyuma kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni. Miongoni mwa hatua hizo ni jitihada za serikali ya Trump za kutambulwa rasmi Israel na nchi za Kiarabu waitifaki wa Washington. Wakati huo huo, Trump hivi sasa yupo tayari kuchukua hatua ya kipekee kabisa ili kuiridhisha tu Morocco ianzishe uhusiano na Israel ili kufanikisha lengo lake hilo na kuonyesha uaminifu wake kwa Tel Aviv na kwa lobi za Kizayuni nchini Marekani. Hatua hiyo ni ile ya kutambua mamlaka ya utawala wa Morocco huko Sahara Magharibi. 

Mkakati wa Trump wa kumshawishi Mfalme wa Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel  

Sahara Magharibi ni eneo lililoko kaskazini magharibi mwa Afrika ambalo limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya Morocco tangu kumalizika ukoloni wa Uhispania mwaka 1974. Harakati ya Polisario ni taasisi ya kisiasa na kijeshi katika eneo hilo. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 kama kundi la muqawama kwa ajili ya kupambana na ukoloni wa Uhispania katika eneo la Sahara Magharibi na kwa lengo la kulikomboa eneo hilo. Polisario iliasisi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahara katika koloni la zamani la Uhispania baada ya nchi hiyo kuondoka Morocco mwaka 1976. Kuanzia hapo Harakati ya Polisario ilianza kupinga hatua ya Uhispania ya kuligawa eneo la Sahara Magharibi kati ya Morocco na Mauritania. 

Eneo la Sahara Magharibi linalopatikana kaskazini mwa Afrika

Aidha mwaka 1979 Mauitania na harakati ya Polisario zilifikia mapatano ya amani; na kwa utaratibu huo sehemu ya kusini ya Jamhuri ya Sahara kwa jina la Wadi el Zahab ilirejeshwa kwa jamhuri hiyo hata hivyo Morocco iliendelea kulikalia kwa mabavu eneo lote la kaskazini mwa Sahara Magharibi kwa jina la al Saguia el-Hamra na kuliunganisha na ardhi yake. 

Kuanzia hapo Harakati ya Polisario ilianzisha mapambano dhidi ya Morocco. Morocco inataka kuwepo mamlaka ya ndani inayofungamana nayo huko Sahara Magharibi, na pia kuwepo bunge la kieneo linalodhibitiwa na serikali kuu ya Morocco. Morocco aidha inadai kuwa kura ya maoni itakayofanyika inabidi ihusiane na suala la eneo hilo kuwa na utawala wa ndani na si kwa ajili ya kujitenga Sahara Magharibi na Morocco. Hata hivyo Harakati ya Polisario inapinga mpango huo na inataka kufanyika kura hiyo ili kuainisha mustakbali wa Sahara Magharibi.   

Harakati ya Polisario 

Kufuatia Trump kuitambua rasmi Sahara Magharibi kuwa sehemu ya Morocco; nchi hiyo sasa inadhani kwamba hatua kubwa imechukuliwa kuelekea kuunganisha ardhi ya eneo hilo na Morocco. Pamoja na hayo, Harakati ya Polisario imesisitiza kuwa, hatua hiyo ya Trump ni kinyume cha sheria. 

Abelqadir Taleb Omar Balozi wa Polisario nchini Algeria ameeleza kuwa, Trump hana milki yoyote huko Sahara Magharibi kiasi cha kuthubutu kutaka kuliunganisha eneo hilo na Morocco; na kwamba hatua yake hiyo inakinzana na sheria zote za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  

 

Tags