Jan 21, 2021 04:44 UTC
  • Zarif: Trump ametupwa katika  jaa la taka za historia, jina la Soleimani litang’ara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema rais aliyeondoka Marekani wa Marekani ametupwa katika jaa la taka za historia.

Katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumatano, Zarif ameashiria jinai zilizotendwa na rais aliyeondoka madarakani wa Marekani Donald Trump, na waziri wake wa mambo ya nje  Mikeo Pompeo hasa mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, “Trump, Pompeo, na wenzao wamefedheheka na wametupwa katika jaa la taka za historia.”

Zarif ameongeza kuwa: “Kitakachobaki na kunawiri ni Kumbukumbu ya Jenerali Soleimani, na maelfu ya wengine ambao waliuawa na kujeruhiwa au kunyimwa matibabu na chakula  na utawala wa Trump kupitia ugaidi wa kiserikali  na jinai dhidi ya binadamu za utawala huo.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemaliza ujumbe wake wa Twitter kwa kuelezea matumaini yake kuwa, pengine watawala wapya nchini Marekani watapata funzo na ibra kutokana na hatima iliyomkumba Trump na wenzake.

Trump

Kauli hiyo ya Zarif imekuja punde baada ya  muhula wa utawala wa Trump kufika ukingoni Jumatano 20 Januari na Joe Biden kuapishwa kama rais wa 46 wa Marekani.

Katika kipindi cha utawala wa miaka minne wa Trump, mtawala huyo mwenye utata alichukua hatua ya kigaidi ya kumuua shahidi Qassem Soleimani na wenzake aliokuwa ameandamana nao mwezi Januari mwaka jana mjini Baghdad. Pompeo alijigamba kuwa alihusika katika maamuzi hayo ya Trump ya kumuaa kigaidi kamanda Soleimani.

Kitendo hicho cha kigaidi cha utawala wa Trump kilifanyika katika fremu ya sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran. Trump alitumai kuwa sera zake hizo zingeilazimu Iran isalimu amri na kuketi kwenye meza ya mazungumzo lakini alifeli kabisa kwani Iran ilishikilia msimamo wake imara. Trump ameondoka kwa fedheha katika uongozi wa Marekani bila kufikia malengo yake haramu dhidi ya Iran.

 

Tags