Feb 22, 2021 14:02 UTC
  • UN: Fikra ya kujiona bora watu weupe na ya Kinazi ni tishio la kimuundo duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuongezwa juhudi za kupiga vita fikra za Kinazi, za kujiona bora Wazungu na watu weupe pamoja na ugaidi wa kizazi na kikaumu.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu António Guterres akisema hayo leo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa kikao cha 44 cha ngazi za juu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuhimiza kuongezwa juhudi za kukabiliana na fikra za Kinazi na kujiona bora watu weupe pamoja na ugaidi unaofanyika kuangamiza kizazi kwa misukumo kama ya kikabila na kikaumu. Amesema, fikra za kujiona bora watu weupe na magenge ya Unazi mamboleo zimeongezeka na sasa zinaelekea kuwa tishio la kimuundo duniani.

Amesema, haki za binadamu ni mstari wa damu yetu. Haki hizo zimejigawanya kwa kiwango sawa kati yetu sote na kwa kiwango hicho hicho ndivyo haki hizo zinavyotuunganisha sote. Mstari wa wokovu wetu ni haki za binadamu kwani hiyo ndiyo njia ya kuweza kutatua migogoro na kuleta amani ya kudumu ulimwenguni. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema: Haki za binadamu ziko katika mstari wa mbele. Haki hizo ndio wenzo wa kuijenga dunia yenye mapenzi na watu kuheshimiana. Haki hizo zinatoa fursa nzuri kwa wote.

Guterres amezungumzia pia athari mbaya za ugonjwa wa COVID-19 kwa suala zima la haki za binadamu na kusema kuwa, ugonjwa huo umezidi kuonesha mianya, ukosefu wa usawa na jinsi wanadamu duniani leo wanavyoishi katika mazingira tete ya kutochungwa haki za binadamu.

Tags