Mar 13, 2021 07:35 UTC
  • UN yataka makubaliano ya usitishaji vita Libya yatekelezwe kikamilifu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka pande zinazopigana nchini Libya kutekeleza kikamilifu makubaliano ya usitishaji vita.

Baraza la Usalama limeeleza katika taarifa kuwa linakaribisha hatua ya bunge la Libya ya kuipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali ya muda ya umoja wa kitaifa itakayoongozwa na waziri mkuu Abdul-Hamid Dabaibah na kuitaka serikali hiyo ijiandae kuitisha uchaguzi tarehe 24 Desemba mwaka huu kama ilivyoafikiwa.

Taarifa ya Baraza la Usalama imesisitiza pia kuhusu udharura wa kuandaa utaratibu wa kuyapokonya silaha makundi yanayobeba silaha nchini Libya na kuyaunganisha pamoja.

Abdul-Hamid Dabaibah

Siku ya Jumatano, bunge la Libya liliwapigia kura ya kuwa na imani nao mawaziri waliopendekezwa kuunda serikali ya muda ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.

Baada ya kupigiwa kura hiyo ya kuwa na imani, mawaziri hao wanatazamiwa kula kiapo siku ya Jumatatu mjini Benghazi.

Kipindi cha serikali ya muda ya umoja wa kitaifa itakayoongozwa na waziri mkuu Abdul-Hamid Dabaibah kitadumu hadi tarehe 24 Desemba na baada ya hapo itaendelea kufanya kazi kwa sura ya serikali ya mshikizo.../

 

Tags