Mar 18, 2021 02:46 UTC
  • Kushindwa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran

Baada ya serikali ya Donald Trump, Rais wa zamani wa Marekani kutangaza kujitoa rasmi katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA mnao Mei 2018, serikali hiyo ilianza kutekeleza vikwazo vikali zaidi katika historia ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fremu ya mchakato wa kile kilichotajwa kuwa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya nchi hii.

Lengo la Trump lilikuwa ni kuilazimisha Iran ikubali matakwa ya kidhalimu ya Marekani lakini ushahidi uliopo unathibitisha wazi kufeli kwa siasa hizo za mashinikizo dhidi ya Tehran. Huu ndio ukweli wa mambo ambao hatimaye waziri mwenye misimamo mikali zaidi katika serikali ya Trump yaani Mike Pompeo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje katika serikali ya Trump ameufikia. Waziri huyo alikuwa na nafasi muhimu katika kuzidisha mashinikizo na hatua za uhasama dhidi ya Iran katika utawala wa Trump. Akizungumza siku ya Jumapili, Pompeo amekiri kuwa serikali ya Washington ilishindwa kabisa kuilazimisha Iran ilegeze misimamo na kuketi na Washington kwenye meza ya mazungumzo.

Kukiri huko kwa kuchelewa kwa Pompeo kunathibitisha wazi kwamba madai yake yote ya huko nyuma kwamba mashinikizo na vikwazo ilivyowekewa Iran vilikuwa na taathira na matokeo yaliyotarajiwa, yote yalikuwa uongo mtupu. Trump na Pompeo walidai kuwa kwa kujitoa katika mapatano ya JCPOA wangeilazimisha Iran kupiga magoti na hatimaye kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia kile walichokitaja kuwa 'mapatano mazuri zaidi'. Pamoja na hayo, mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya Iran ambayo yaliendelea kwa zaidi ya miaka miwili na nusu yaligonga mwamba na kushindwa kufikia malengo yaliyokuwa yakifuatiliwa na utawala wa Trump.

Mike Pompeo

Jambo hilo lilimpelekea kiongozi huyo mwenye kiburi na utata mwingi kukabiliwa na ukosoaji mkubwa wa ndani na nje ya Marekani. Wakosaji wake walimtuhumu kwa kutokuwa na mipango na stratijia ya wazi ya kukabiliana na Iran na kuchochea mivutano ya kieneo isiyokuwa na maana pamoja na kuitenga Marekani na washirika wake wa kieneo na kimataifa. Ukosoaji huo wa siasa za Trump kuhusu Iran haukufanywa tu na washindani na vilevile washirika wa kigeni wa Marekani bali hata na viongozi na wajuzi wa mambo ndani ya Marekani yenyewe.

Paul Pillar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema: Kuna ushahidi mwingi unaowafanya wajuzi wa mambo kufikia yakini kwamba hatua za serikali ya Trump za kuongeza mashinikizo kwa ajili ya kuilzimisha Iran isalimu amri zimeshindwa. Ukweli huu unatiliwa nguvu pale tunaposhuhudia hata wale waliokuwa waungaji mkono wakubwa wa stratijia hiyo wakikiri kuwa imeshindwa kufukia malengo yaliyokusudiwa.

Suala hilo linaweza kuwa ni funzo muhimu kwa Joe Biden, rais wa hivi sasa wa Marekani kwa lengo la kumfanya asikariri makosa yaliyofanywa huko nyuma na serikali ya Trump. Kabla ya kuingia White House, Biden aliahidi kwamba mara tu baada ya kuingia ikulu hiyo angeweka pembeni siasa za Trump kuhusiana na Iran na kuirejesha Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Licha ya madai hayo na baada ya kupita miezi miwili tokea aingie madarakani hakuna chochote cha maana alichokifanya hadi sasa kuhusiana na ahadi alizotoa kwa Wamarekani kuhusu jambo hilo, bali amekuwa akitekeleza siasa zile zile za mashinikizo na vikwazo za mtangulizi wake Trump dhidi ya Iran. Suala hilo lilionekana wazi hivi karibuni ambapo alichukua hatua ya kuiwekea Iran vikwazo vipya.

Paul Pillar

Kwa mujibu wa Kaitlin Johnstone, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, Biden anaendeleza kivitendo siasa zile zile za Trump dhidi ya Iran.

Ni wazi kuwa siasa hizo hazitakuwa na natija nyingine ghairi ya kufeli na kuifedhehesha Marekani mbele ya Iran. Hii ni pamoja na kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata uzoefu na mafanikio maklubwa katika kukabiliana na siasa za chuki na uadui za Marekani kupitia vikwazo na mashinikizo ya juu dhidi yake. Kwa msingi huo ni wazi kuwa Iran haitakubali wala kusalimu amri mbele ya siasa zisizo za kimantiki za Marekani zikiwemo za kuitaka Iran ianze kutekeleza tena majukumu yake ya JCPOA bila yenyewe kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Tehran.

Tags